Na Mwandishi wetu,
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Bukoba imetoa hati ya kumkamata na
kumfikisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Dennis Mwira kwa kosa la
kupuuza amri ya Mahakama.
Amri hiyo imetolewa Novemba 2 mwaka huu na Hakimu Mkazi,
Samuel Maweda baada ya mkuu huyo wa wilaya kukaidi amri ya kuachia ng'ombe 541
wa wafugaji wa kitongoji cha Rwenkuba wilayani humo waliokamatwa isivyo halali.
Septemba 22, mahakama hiyo ilitoa amri ya ng'ombe hao
kuachiwa baada ya wananchi kufungua shauri la madai namba 21/2017 kupinga
ng'ombe wao kukamatwa katika eneo lenye mgogoro unaoendelea katika mahakama kuu
kitengo cha ardhi kwa shauri namba 14/2017.
Wakili wa wananchi 143 waliofungua kesi mahakamani, Danstan
Mutagahywa Alhamisi alisema baada ya Mkuu wa Wilaya na mdaiwa mwenzake,
Ladislaus Martin ambaye ni Meneja wa Ranchi ya Misenyi baada ya kukaidi
kutekeleza amri hiyo, waliwasilisha ombi la watu hao kukamatwa kwa kudharau
amri ya Mahakama.
“Siyo tu wamekaidi kutekeleza amri halali ya Mahakama, DC na
mwenzake pia wamegoma kupokea hati za wito na kufikia hatua ya kumkamata na
kumweka mahabusu dalali wa Mahakama aliyepewa amri ya kutekeleza zoezi la
kurejesha ng'ombe wanaoshikiliwa isivyo halali," alisema Mutagahywa.
Alisema amri hiyo ilitarajiwa kufikishwa ofisini kwa Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), wa Kagera jana Ijumaa Novemba 3.
Alimtaja dalali wa Mahakama aliyekamatwa na kuswekwa mahabusu
kwa amri ya DC Oktoba 31, kuwa ni Ignatus Bashemela aliyeachiwa huru baada ya
yeye kuwasilisha suala hilo ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera
akionyesha nyaraka halali za Mahakama kuhusu jambo hilo.
Wakati shauri la madai dhidi ya DC na mwenzake Ladislaus
likitarajiwa kusikilizwa mara watakapokamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama,
ile ya ardhi ambayo bado inatajwa mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Bukoba, Seif Musa, itatajwa tena Machi 8, 2018.
Kauli ya Mkuu wa Wilaya:
Akizungumza kwa njia ya simu mkuu huyo wa wilaya amesema
aliagiza kukamatwa kwa dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambaye
alifika bila kutoa taarifa yoyote kwa mamlaka za Serikali.
Alisema kuwa mtu huyo alikwenda moja kwa moja katika eneo
wanapotunzwa ng'ombe zaidi ya 80 walioingizwa nchini kutoka Uganda bila
kufuata utaratibu.
"Hilo suala la dalali wa Mahakama nalisikia kwako
niliyeagiza akamatwe ni dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambao
tumewakamata alifika bila kufuata taratibu nikaagiza akamatwe,"amesisitiza
Kanali Mwila.
Ameongeza kuwa alikamata ng'ombe zaidi ya 400 na wamiliki
wake kutoka Uganda walilipa faini na kuwarudisha kwao na kubaki ng'ombe 88
aliosema alipata taarifa kuwa wanataka kuchukuliwa kwa nguvu na watu ambao hata
hawakupita kwenye ofisi yake.
Pia alisema hana taarifa yoyote ya kuwepo kwa hati ya
Mahakama dhidi yake na kuwa anaendelea kuwasaka raia wawili wanaodaiwa
kushirikiana na wafugaji wa Uganda kuingiza mifugo hiyo bila utaratibu.
No comments:
Post a Comment