Na Muhidin Amri,
Songea.
Songea.
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Ruhuwiko
mkoani Ruvuma inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedi ya 401
Tembo Kanda ya kusini, wametakiwa kusoma kwa bidii na kuzingatia masomo yao darasani
ili waweze kutimiza ndoto ya kuwa viongozi bora watakao weza kulitumikia taifa
hili.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa
wiki na Mkuu wa mafunzo na utawala wa Brigedi hiyo Kanal John Mwaipaya wakati
akizungumza na wananchi, walimu na wazazi katika mahafali ya 22 ya kidato cha
nne shuleni hapo.
Aidha alisema kuwa lazima mwanafunzi
atambue kwamba analo jukumu la kusoma kwa kujituma ili aweze kufanya vizuri
katika mitihani yake ya mwisho jambo ambalo litamsaidia kuwa na uhakika wa
ajira na uwezo wa kukabiliana na
changamoto mbalimbali katika maisha ya kila siku.
Pia Kanal Mwaipaya aliwataka
wanafunzi wa shule hiyo hasa watoto wa kike kujiheshimu na kujaribu kuzuia
tamaa za miili yao kwa kujiepusha na vitendo vya anasa ambavyo vinachangia kuwa
katika hatari ya kupata mimba na ugonjwa wa ukimwi.
Meneja wa shule hiyo, Luten Kanal
Kassian Chausi aliwataka wazazi na walezi kuwa andaa vyema watoto wao kwa
kuwapeleka shule kwa muda muafaka ili hapo baadaye waweze kuwa na sifa bora
hata ya kujiunga na vikosi vya ulinzi na usalama Jeshini.
Kwa mujibu wa Chausi alieleza
kuwa jamii lazima itambue kuwa zama hizi sio za ujanja ujanja na kubebana bali
kila mmoja ataishi kwa kufanya kazi halali itakayompatia kipato cha
kila siku badala ya kuendelea kuishi kwa mazoea.
Alitolea mfano, hivi karibuni
Serikali kupitia Wizara ya ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa imetangaza nafasi
za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana na kuweka vigezo, hata
hivyo katika hali ya kusikitisha bado vijana wengi wa mkoa wa Ruvuma waliojitokeza
kuomba nafasi hizo walikosa sifa na nafasi kuchukuliwa na vijana kutoka nje ya
mkoa.
Sambamba na hilo amewaonya pia vijana
hao kuacha kuishi maisha ya sterehe badala yake wahakikishe wanatumia muda
wao kusoma kwa bidii ili kujiandaa na maisha yao ya baadaye kwani maisha ya uraiani
ni magumu tofauti na vile wanavyofikiria.
No comments:
Post a Comment