Na Muhidin Amri,
Songea.
KAMPUNI ya Kambas Group of Companies,
inayofanya utafiti wa makaa ya mawe katika kitongoji cha Mipeta na Manyamba
kata ya Muhukuru Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa msaada
wa mifuko ya saruji 150 na bati 100 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya
madarasa, nyumba mbili za walimu na ofisi ya shule ya msingi Mipeta iliyopo
wilayani humo.
Mwanzoni mwa mwezi huu upepo mkali ulioambatana
na mvua uliezua paa katika baadhi ya madarasa, ofisi za walimu pamoja na nyumba
mbili za walimu hali iliyosababisha wanafunzi kuanzia darasa la kwa kwanza hadi
sita kulazimika kusomea vyumba viwili vya madarasa huku walimu walioezuliwa
nyumba zao za kuishi wakiomba hifadhi ya kulala kwa walimu wenzao na wenyeji wa
kitongoji hicho.
Akikabidhi msaada huo jana kwa Mkuu
wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yahaya Yusuph alisema
wameamua kutoa vifaa hivyo vya ujenzi ikiwa ni mkakati wa kampuni yake kuunga
mkono mpango wa Serikali ya Rais Dokta John Pombe Magufuli ya kutoa elimu bure,
hivyo yeye kama mdau wa maendeleo ameona ni vyema kuchangia vifaa hivyo ili
watoto hao waweze kuendelea na masomo katika mazingira mazuri.
Alisema kuwa msaada huo alioutoa una thamani
ya shilingi milioni 5.5 ambazo zitawezesha kurudisha miundombinu ya shule hiyo
kama ilivyokuwa hapo awali ili walimu na wanafunzi waweze kuondokana na adha
hiyo wanayoipata sasa.
Alisema kuwa baada ya kuona tatizo
hilo kupitia kituo kimoja cha Televisheni aliguswa na kuamua kutoa msaada huo
wa mabati na saruji vyote vikiwa na thamani hiyo kwa lengo la kuweza kupunguza
madhara hayo yaliyojitokeza.
Kadhalika ameyataka makampuni mengine
ndani na nje ya nchi na wale watu wenye uwezo kujitokeza kuisaidia shule hiyo
vifaa na mahitaji mengine, na sio kuiachia Serikali peke yake ambayo
inakabiliwa na majukumu mengi ya utekelezaji wa maendeleo ya wananchi.
Akipokea msaada huo mkuu wa wilaya ya
Songea, Palolet Mgema mbali na kuishukuru kampuni hiyo kwa msaada wake alisema
kuwa upepo huo ambao uliambatana na mvua ulisababisha madhara makubwa
hata kwa wananchi ambapo nyumba 29 ziliezuliwa na nyingine kuta zake kuanguka.
Mgema aliongeza kuwa mahitaji halisi
kwa madhara yaliyotokea katika tukio hilo ni bati 330 na saruji mifuko 380 hata
hivyo kampuni hiyo imetoa nusu ya sehemu ya mahitaji yao ambapo ametoa wito kwa
watu mbalimbali kuangalia uwezekano wa kusaidia vifaa vingine vitavyoweza
kusaidia kurudisha miundombinu ya shule hiyo katika hali yake ya kawaida kama ilivyokuwa
hapo awali.
No comments:
Post a Comment