Na Clarence Nanyaro – NEC
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage amewataka Wasimamizi na Wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi hapa nchini, kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa
katika maamuzi mbalimbali wanayofanya yenye maslahi kwa pande zote ili
kuendeleza amani na utulivu tulionao.
Akizungumza na Wasimamizi wa uchaguzi
katika Manispaa ya Moshi, Jaji Kaijage alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho
vyama vya siasa vinashiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani ambao
utafanyika Novemba 26 mwaka huu, ni muhimu kwa wasimamizi wa uchaguzi
kuhakikisha kuwa maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni yanazingatiwa ili
kuepusha uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.
Jaji Kaijage ambaye yuko katika ziara
ya kutembelea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kushuhudia utekelezaji wa
maadili hayo katika kampeni za uchaguzi huo.
Amewataka wasimamizi kuhakikisha
kuwa vifaa vyote ambavyo vinahitajika ili uchaguzi uweze kufanyika viwe vimepatikana
na vile ambavyo havijapatikana wa wasiliane na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili
kasoro zinazobainika ziweze kupatiwa ufumbuzi mapema kabla ya siku ya uchaguzi
kuwadia.
Kadhalika alitoa wito kwa wasimamizi
wa uchaguzi huo kuhakikisha kuwa siku ya upigaji kura ulinzi unaimarishwa
katika vituo vya kupigia kura, lakini usiwe ulinzi wa kuwatia wananchi hofu
wakashindwa kufika katika vituo vya kupigia kura kuchagua viongozi wanaowataka
ili waweze kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment