Na Mathias Canal,
Mtwara.
Mtwara.
NAIBU Waziri wa kilimo, Mary Machuche
Mwanjelwa amemtaka Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Mtwara, kukamilisha haraka
kazi ya uchunguzi kwenye bodi za vyama vya ushirika mkoani humo ili kubaini
sababu zilizosababisha kuuzwa kwa magunia kiholela bila kufuata taratibu.
Alisema kuwa kumalizika kwa uchunguzi
huo kutarahisisha kuchukuliwa haraka hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika
kukiuka sheria namba 17 ya vyama vya ushirika.
Naibu Waziri huyo alitoa agizo hilo
wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Chiungutwa,
Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara mara baada ya kugundua kuwa kuna viashiria vya
ukiukwaji wa taratibu katika upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia korosho wakati
wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Sambamba na hilo Mwanjelwa wakati
wote alipokuwa kwenye mkutano huo ameshuhudia malalamiko kutoka kwa wakulima wa
zao la Korosho wa Chama cha Ushirika cha Masasi-Mtwara Cooperative Union Limited
(MAMCU) kuhusu ucheleweshwaji wa upatikanaji wa magunia hayo kutoka kwa mzabuni,
mapungufu ya kilo kati ya PDA na WHRs ghala kuu, ikiwa ni pamoja na kuchelewa
kwa malipo ya wakulima kwa njia ya benki kutoka kwa wanunuzi.
Katika ziara yake hiyo kilio cha
wananchi wengi na wakulima walisisitiza zaidi kuhusu kukosekana kwa magunia
hayo huku wakieleza kuwa wakati mwingine kuchelewa kufika au kutowafikia kabisa
jambo ambalo linachangia kupunguza thamani ya zao la korosho.
“Nataka Mrajisi ufanye na ukamilishe
kazi yako ya uchunguzi haraka na baada ya kuipata taarifa hiyo hatua stahiki
zitachukuliwa kwa wale wote watakaogundulika kukiuka sheria za nchi”, alisema
Mwanjelwa.
Mbali na agizo hilo Naibu Waziri huyo
wa Kilimo pamoja na Wabunge wa Mkoa huo walipata nafasi ya kujionea mnada wa
tano wa ununuzi wa zao la Korosho unavyoendelea.
Hata hivyo mnada wa tano ulishuhudiwa
Kilogramu 7,524,104 za Korosho zikiuzwa kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 30.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanjelwa
alisema kuwa Wizara yake itayafanyia kazi haraka mapendekezo ya tume iliyoundwa
na Mkuu wa Mkoa huo, Gelasius Gasper Byakanwa kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo
mzima wa magunia hayo pamoja na upatikanaji wake.
No comments:
Post a Comment