Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
Namtumbo.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea
kuweka miundombinu ya uhakika katika sekta ya elimu hapa nchini, ili kuweza kutoa
fursa kwa watoto waliopo shuleni waweze kusoma vizuri na kutimiza malengo yao
ya maendeleo ya maisha ipasavyo.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana
wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Nasuli wilayani Namtumbo mkoa
wa Ruvuma huku akiwataka wazazi watekeleze jukumu la kila mtoto mwenye umri wa
kwenda shule ni lazima apelekwe shuleni ili aweze kusoma.
Aidha alifafanua kuwa mpango wa Serikali
hivi sasa ni kuhakikisha kwamba kila kwenye shule ya kidato cha kwanza
hadi cha nne kunakuwa na shule ya kidato cha tano, ikiwa ni lengo la
kuwarahisishia watoto wanaofanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato
cha nne waendelee na masomo yao jambo ambalo litasaidia kupata vijana
wengi watakaokwenda vyuo vikuu.
Kwa mujibu wa Waziri mkuu alieleza
kuwa katika mkakati huo Serikali imetoa nafasi kwa watu binafsi na mashirika
mbalimbali kuanzisha vyuo vikuu ili watoto wengi zaidi wajiunge na vyuo hivyo na
hatimaye Taifa liweze kupata wasomi wengi zaidi watakaotumikia nchi yetu.
Alisema kuwa katika kufanikisha
malengo hayo wametenga zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kununua seti
za masomo na tayari zimeshaanza kusambazwa katika shule mbalimbali hapa nchini
ili kuwarahisishia watoto kuwa na uelewa mkubwa katika masomo yao.
Hali kadhalika Majaliwa amewataka
watoto kuwa wavumilivu wakati huu ambao Serikali inaendelea kutekeleza mpango
huo na kuwaasa watoto hasa wasichana wajiepushe na vitendo viovu kama vile
uasherati ambavyo vinaweza kusababisha kupata mimba na kukatisha ndoto zao za
kuendelea na elimu.
Pia alitoa onyo kwa wanaume kuacha
tabia ya kuwalaghai watoto hao huku akionya kuwa mtu yoyote atakayekamatwa
akifanya mapenzi na mwanafunzi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha
kuona wilaya ya Namtumbo kwa muda mrefu imekuwa miongoni mwa wilaya zenye
rekodi mbaya ya wanafunzi kupata ujauzito na utoro ambapo amewaagiza viongozi
wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba wanadhibiti hali hiyo kwa kuwafikisha
Mahakamani watuhumiwa ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama
hiyo.
No comments:
Post a Comment