Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AGIZO limetolewa kuwa fisadi au mwizi yeyote atakayejitokeza
kuiba sehemu ya fedha shilingi milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali, kwa
ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, haraka achukuliwe hatua za kisheria asionewe
huruma.
Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme alitoa agizo hilo juzi
akimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye kusimamia ipasavyo matumizi ya
fedha hizo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa, wakati alipokuwa ametembelea
eneo la ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa lengo la kujionea ujenzi ambao
unaendelea kufanyika huko.
Alisema kuwa fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali ya
awamu ya tano zinalenga kuboresha huduma ya afya katika kata hiyo ili wananchi
wanaoishi huko waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa kilometa
35 kwenda hospitali ya wilaya kutafuta matibabu pale wanapougua.
Mndeme alifafanua kuwa ushirikiano katika kukamilisha kazi
hiyo kati ya wananchi na viongozi wanaosimamia ujenzi huo ni muhimu uzingatiwe
ili ujenzi wa majengo husika uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa.
“Hizi fedha ni za Watanzania, Mheshimiwa Rais Dokta John
Pombe Magufuli katuletea hapa tuweze kuboresha mazingira ya kutolea huduma ya
afya na hatimaye wanambinga waweze kunufaika na matunda ya Serikali yao ya wamu
ya tano”, alisema Mndeme.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Kihungu aliwataka pia
kutovamia eneo la ujenzi wa kituo hicho ikiwemo pasitokee wizi wa vifaa vya
ujenzi ambavyo vimenunuliwa na kuletwa hapo kwa ajili ya kukamilisha shughuli
za ujenzi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye
alimhakikishia Mkuu wa mkoa huyo kwamba atasimamia ipasavyo maelekezo yote
yanayopaswa kutekelezwa katika shughuli za ujenzi wa kituo cha afya Kalembo ili
kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Hata hivyo ujenzi huo unatekelezwa kwa kujenga jengo la
upasuaji, maabara, nyumba ya mganga, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya akina
mama na watoto na kwamba ujenzi wake unapaswa kukamilika ifikapo Disemba 30
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment