Na Mwandishi Wetu,
RAIS Dokta John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri (DED) Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Abdallah Mussa
kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi wilayani humo.
Kutenguliwa kwa uteuzi wa Mkurugenzi huyo leo Alhamisi
Novemba 9 mwaka huu kumefanyika siku tatu baada ya Rais Magufuli kutengua
uteuzi wa wakurugenzi wengine wawili.
Taarifa ya Rebecca Kwandu, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano
Serikalini katika Ofisi ya Tamisemi imesema kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ndiye aliyotoa taarifa ya
kutenguliwa kwa uteuzi huo leo mjini Dodoma.
Alisema kwamba kutokana na hatua hiyo uteuzi wa Mkurugenzi
mwingine utafanyika hapo baadaye.
Rais Magufuli Novemba 6 mwaka huu alitengua uteuzi wa
wakurugenzi wa halmashauri za Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa
Halmashauri ya Bukoba, Mwamtumu Dau.
Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa
Barabara zilizopokelewa kwenye halmashauri zao walipoulizwa na Rais Magufuli
wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Alipoitwa mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi cha fedha
zilizopokelewa katika halmashauri kwa ajili ya mfuko huo, Mwantumu alijibu kuwa
ana idara nyingi anazozisimamia hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila
kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina huku akiongeza kuwa hawezi kusema
uongo.
Dokta Magufuli katika mkutano huo alisema kuwa amewasamehe
lakini baadaye Ikulu ilitoa taarifa ikieleza Rais ametengua uteuzi wao.
No comments:
Post a Comment