Na Albano Midelo,
Songea
WAUMINI wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Augustino
Mjimwema Songea Dayosisi ya Ruvuma, wamechanga zaidi ya shilingi milioni 57
kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.
Katibu wa kanisa hilo Dokta Daniel Mtamakaya alisema ili waweze
kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo, zinahitajika zaidi ya shilingi milioni 186.
Dokta Mtamakaya alisema kuwa kanisa hilo limefanikiwa pia kuchangisha
zaidi ya shilingi milioni 33 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuezeka kanisa na kwamba
kinachohitajika hivi sasa ni shilingi milioni 15 ambazo ni gharama za kumlipa
fundi.
Kwa mujibu wa Katibu huyo aliongeza kuwa wameweza kujenga
shule ya Jumapili (Sunday School) ambayo ujenzi wake utagharimu zaidi ya
milioni tano hadi utakapokamilika miundombinu yake.
“Mara tu baada ya kuezeka kanisa jipya, kanisa dogo
linalotumika hivi sasa, litabadilishwa matumizi ili iweze kuwa nyumba ya kuishi
wahudumu wa kanisa na kuweza kuepuka kuwalipia pango ambalo hugharimu fedha
nyingi kanisa”, alisema.
Akizungumza baada ya kupata taarifa ya ujenzi wa kanisa hilo,
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma Mhashamu Raphael Haulle aliwapongeza
waumini wake kwa kugharamia ujenzi huo na kuanzisha shule ya watoto.
Askofu Haulle alieleza kuwa kanisa linaendelea kufanya
jitihada ya kutafuta wafadhili wa ndani na nje ya nchi ili kuharakisha ujenzi huo
ambao asilimia kubwa zimetumika nguvu za waumini wenyewe.
“Najaribu kuwasiliana na wafadhili wa ndani na nje ya nchi, baadhi
ya wafadhili toka nchini Ujerumani wamefika hapa kuangalia kanisa hili, naamini
Mungu atatupa fedha za kuezeka na kukamilisha ujenzi wa kanisa hili’’, alisema Askofu
Haulle.
Vilevile alitoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kutoka
ndani na nje ya nchi kutoa mchango wowote ili kuweza kukamilisha ujenzi wa
kanisa hilo.
No comments:
Post a Comment