Sunday, November 19, 2017

OFISI YA DED HALMASHAURI MJI WA MBINGA LAWAMANI WANAFUNZI MASUMUNI WASOMEA NJE YA MADARASA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma imeshushiwa tuhuma kwa kutelekeza baadhi ya miradi ya maendeleo ya wananchi kwa kushindwa kuchangia vifaa vya kiwandani pale inapofikia hatua ya kufanya hivyo.

Christine Mndeme Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Frank Mgeni ambaye ni diwani wa kata ya Mbinga mjini B, aliibua tuhuma hiyo katika kikao cha baraza la Madiwani lililoketi hivi karibuni mjini hapa na kueleza kuwa miradi hiyo ya wananchi halmashauri imekuwa ikishindwa kutekeleza hilo licha ya wananchi kuchangia nguvu zao kwa asilimia kubwa.

Mgeni alisema kuwa hata ujenzi wa choo katika shule ya msingi Mbinga iliyopo mjini hapa ambacho wananchi wamejitolea kwa nguvu zao kukijenga, licha ya kupeleka ombi kwa uongozi husika wa halmashauri hiyo ili waweze kupewa vifaa vya kiwandani kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo ni muda mrefu sasa umepita hakuna utekelezaji uliofanyika.

“Kwa mfano mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa choo cha shule ya msingi Mbinga chenye matundu nane ni muda mrefu nimekuwa nikipeleka maombi ya kutaka wananchi wangu wapewe vifaa vya kiwandani ili tuweze kufikia hatua ya mwisho kumaliza ujenzi hakuna majibu ya uhakika ninayo yapata kila siku nimekuwa nikipigwa kalenda”, alisema Mgeni.

Naye diwani wa viti maalum Mbinga mjini, Mary Yapesa aliongeza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga inashindwa hata kuwaonea huruma watoto wa shule ya msingi Masumuni iliyopo mjini hapa ambapo ni muda mrefu wamekuwa wakisomea nje ya vyumba vya madarasa, baada ya jengo lenye vyumba vitatu kubomolewa ili viweze kujengwa upya kutokana na jengo lililokuwa hapo awali kujenga nyufa na kuhatarisha usalama wa watoto hao.

“Ni muda mrefu sasa unapita watoto wale hawana sehemu ya kusomea wamekuwa wakisoma nje ya madarasa na mwakani watoto wengine wanaingia darasa la kwanza na kipindi cha masika ndiyo kinaanza lakini ujenzi wake hakuna kitu kinachoendelea pale tunaomba mambo muhimu kama haya yapewe kipaumbele”, alisema Yapesa.

Wakichangia hoja kwa nyakati tofauti nao Madiwani wenzake walisema wanataka halmashauri ya mji wa Mbinga iunge mkono kazi za maendeleo zinazofanywa na wananchi kwa wakati hasa pale wanapofikia hatua nzuri ya ujenzi wa miradi hiyo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Kwa upande wake alipotakiwa kutolea ufafanuzi mbele ya baraza hilo Afisa mipango wa halmashauri ya mji huo, Donald Msigwa alikiri kuchelewa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kutokana na halmashauri hiyo kutotoa vifaa vya kiwandani huku akiongeza kuwa utekelezaji huo utafanywa kulingana na makusanyo ya mapato ya fedha watakazofanikiwa kukusanya.

No comments: