Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
Namtumbo.
WAGANGA Wakuu wa mikoa na wilaya hapa
nchini wameagizwa kuendelea kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa
sekta ya afya ambao wanajihusisha na vitendo vya wizi wa dawa za Serikali.
Kassim Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliojumuisha wananchi pamoja na viongozi wa wilaya ya
Namtumbo katika uwanja wa michezo mjini hapa.
Alisema kuwa katika kuimarisha sekta hiyo
Serikali imeongeza bajeti ya fedha kutoka shilingi bilioni 32 hadi kufikia
bilioni 220 kwa mwaka huku akisisitiza dhamira ya Serikali ina lengo la kuondoa
usumbufu wa upatikanaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake
za Serikali kote nchini.
Aliongeza kuwa baadhi ya watumishi wa
afya wamekuwa chanzo cha matatizo ya upungufu wa dawa za binadamu katika sekta
hiyo kutokana na tabia ya wizi ambapo alionya kwamba watumishi wa aina hiyo
hawatafumbiwa macho watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Nawaagia Waganga wakuu wa mikoa na
wilaya hapa nchini kuwashughulikia watumishi wote wanaojihusisha na wizi wa
dawa za Serikali katika maeneo ya kutolea huduma za afya”, alisisitiza Waziri Mkuu.
Pia aliwahamasisha Madiwani
kuhamasisha wananchi wao kushiriki kikamilifu katika kazi ya ufyatuaji tofali
kwa ajili ya kutekeleza mpango wa ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji na kituo
cha afya kwa ngazi ya kata.
Alisema kuwa mpango huo ukifanikiwa
wananchi watapata maeneo bora ya kutolea huduma bora za afya na Serikali
itahakikisha inapeleka fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
Pia aliwataka maafisa ugani kote
nchini kuhakikisha wanatembelea wakulima mashambani ili kufahamu matatizo waliyonayo
na aina ya mazao yanayostawi vizuri katika maeneo wanayoishi pamoja na kutafuta
masoko ya mazao hayo yanayozalishwa katika husika badala ya kutumia muda mwingi
kukaa Ofisini.
Alibainisha kuwa Serikali itaendelea
kutafuta makampuni mengi zaidi kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima ikiwemo
mbaazi na korosho huku akisisitiza maafisa hao kutumia utaalam wao kuwasaidia
wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kisasa ili waweze kupata mazao
mengi.
No comments:
Post a Comment