Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
Mbinga.
KAMPUNI ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa
Wilayani Mbinga (MCCCO) mkoa wa Ruvuma, inalazimika kuwatumia wazabuni waliopo
nje ya nchi kusambaza magunia ya kuhifadhia kahawa safi ambayo inakobolewa
kiwandani hapo, kutokana na mzabuni aliyepewa kazi hiyo hapa nchini kushindwa kufanya
kazi hiyo.
Aidha kufuatia hali hiyo, Serikali imeombwa
kuruhusu wazalishaji wa magunia hayo wawe wengi ili kuweza kunusuru hali hiyo
na kufanya kahawa inayokobolewa hivi sasa kiwandani hapo iweze kuhifadhiwa
katika mazingira mazuri.
Injinia Rabiel Ulomi ambaye ni Meneja
uzalishaji wa kiwanda hicho, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza ofisini
kwake na mwandishi wa habari hizi juu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao la
kahawa wilayani humo.
Ulomi alifafanua kuwa kazi ya
usambazaji wa magunia hayo ilikuwa ikifanywa na kampuni ya Mohamed Enterprises kutoka
jijini Dar es salaam, kwa miaka mingi lakini hawajui kwa nini mzabuni huyo
aliyepewa dhamana hiyo amesitisha huduma ghafla ya kutosambaza magunia hayo.
“kuhusu changamoto hii ya uhaba wa
magunia ni kweli tunayo, hili tatizo limejitokeza kwa ukubwa hasa kwa mwaka huu
kwa sababu mzalishaji mkubwa wa magunia tunayemtegemea hapa kwetu ni Mohamed
Enterprises kutoendelea kutoa huduma na hatujui kwa nini amesitisha licha ya
uongozi wetu kuwasiliana na bodi ya kahawa”, alisema Ulomi.
Alifafanua kuwa magunia wanayotumia
sasa inawalazimu kuagiza kutoka India na kwamba tatizo hilo wakati mwingine limekuwa
linakwamisha hali ya uhifadhi wa kahawa katika mazingira bora.
“Tunafikiri kwamba kwa sera za
Tanzania ya viwanda ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa sana na kufanyiwa
utekelezaji ili kuweza kuachana na mfumo huu wa kuagiza malighafi nje ya nchi”,
alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine Meneja huyo
wa uzalishaji kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga, aliwataka pia wadau wa kahawa
wilayani hapa kujitokeza kwa wingi na kujenga maghala ya kuhifadhia zao hilo
ili kuweza kuondokana na tatizo la upungufu wa maghala ambalo linaikabili
wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment