Wagonjwa wanaodaiwa kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na sumu wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Mji wa Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATU 72 ambao ni Wakazi wa kitongoji
cha Kipika kata ya Matarawe katika Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamenusurika
kupoteza maisha baada ya kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na
sumu.
Aidha imeelezwa kuwa tukio hilo
lilitokea Novemba 19 mwaka huu majira ya mchana, ambapo kinywaji hicho
walikunywa wakiwa kwenye sherehe (Harusi) iliyokuwa ikifanyika katika kitongoji
hicho.
Mmoja kati ya wagonjwa waliolazwa
katika wodi ya wanaume hospitalini hapo, Chirwa Mohamed Hassan akizungumza na
mwandishi wetu alisema kuwa baada ya kunywa kinywaji hicho na masaa machache
kupita, ghafla yeye na wenzake walijikuta tumbo linauma na kuanza kuharisha
mfululizo ndipo walikimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.
“Baada ya kula chakula tulipewa togwa
tulikuwa tunakunywa masaa machache yalipopita ndipo tumbo lilianza kuuma na
kuharisha lakini baada ya kuwahi hapa hospitalini, tunawashukuru waganga kwa
kutupatia matibabu kwa uharaka na sasa tunajisikia kuna unafuu kidogo”, alisema
Hassan.
Naye Cecilia Venant Ndomba ambaye
amelazwa katika wodi ya wanawake alifafanua kuwa yeye alipomaliza kunywa togwa
hiyo tumbo lake lilianza kuuma na kuanza kutapika ghafla.
“Kufikia majira ya saa kumi jioni
hapa hospitalini wakati tunaletwa tulikuwa hatujuani mimi nilipoteza fahamu
tumbo langu lilikuwa linanyonga sana”, alisema Ndomba.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa
hospitali ya Mji wa Mbinga, Festo Mapunda alithibitisha kuwapokea wagonjwa hao
na kueleza kuwa mpaka sasa yeye na timu yake ya wataalamu wa hospitali hiyo
inaendelea kufanya uchunguzi, ili waweze kubaini chakula na vinywaji
walivyokula kama vilikuwa na sumu au la na taarifa zitatolewa tena baadaye.
“Wagonjwa walioripotiwa mpaka sasa ni
72 tunaendelea kuchukua sampo ya vyakula katika eneo lile la sherehe ili tuweze
kufanya utafiti wa kina, lakini tumebaini mpaka sasa hawa wagonjwa wamekula
uchafu ambao ulikuwa kwenye chakula”, alisema Mapunda.
Mapunda alisema kuwa kati ya wagonjwa
hao waliolazwa katika hospitali hiyo 46 ni wanawake, 23 ni wanaume na watatu ambao
ni wanaume pia walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
No comments:
Post a Comment