Na Mwandishi wetu,
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba maandalizi ya
vifaa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani, unaofanyika katika kata 43
yamekamilika na awamu ya pili ya vifaa hivyo vitaanza kusafirishwa kesho Ijumaa
kwenda katika kata husika.
Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC Kailima Ramadhani alisema kuwa vifaa
vitakavyosafirishwa kuanzia kesho ni maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa
wasimamizi wa vituo, makarani waongozaji pamoja na mfano wa karatasi za
kupigia kura.
Ramadhani alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya kusafirisha
vifaa hivyo ulifanywa na tume wakati wa mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi
ambayo yalifanyika mjini Dodoma ambavyo vilitumika wakati wa uteuzi wa wagombea
udiwani katika kata zote.
“Napenda kuwahakikishia umma kwamba tume imejipanga vizuri kwa
ajili ya uchaguzi huu na maandalizi ya kupeleka vifaa katika kata husika yako
vizuri na awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa vitapelekwa kesho”, alisema
Ramadhani.
Alisema awamu ya tatu ya usafirishaji wa vifaa itahusisha vifaa
vichache ambavyo ni karatasi za kupigia kura pamoja na fomu za kutangazia
washindi ngazi ya kituo na ngazi ya kata.
Naye Mkurugenzi wa Manunuzi, Ugavi na Logistiki wa NEC Eliud
Njaila, alisema kwamba NEC imepeleka vifaa vya kutosha katika vituo vyote 893 vilivyoko
katika kata 43 na hakutakuwa na upungufu wowote.
Alieleza kwamba katika awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa,
wameweka na mfano wa karatasi za kupigia kura ili wadau ambavyo ni vyama vya
siasa vijiridhishe kuhusu karatasi hizo hivyo zitakavyokuwa pamoja na kufanya
uhakiki wa majina wa wagombea wao.
“Tunaamini kwamba vyama vya siasa vitahakiki majina ya
wagombea wao kwa kila kata ili kama kuna masahihisho wayalete mapema na NEC
iweze kufanya masahihisho haraka wakati wa kuchapa karatasi halisi za kupigia
kura,” alisisitiza Njaila.
Njaila pia aliwataka wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya
kuwatumia maafisa boharia katika kupokea na kutunza vifaa hivyo.
Alisema wataalamu hao pia ndio watumike pia kusafirisha vifaa
hivyo kwa kuwa wao wana ujuzi wa namna ya kutunza na kugawa vifaa.
Alifafanua kuwa iwapo wasimamizi wa uchaguzi watawatumia
maafisa ugavi ni wazi kuwa hakutakuwa na malalamiko ya kupungua kwa vifaa
katika vituo vya kupigia kura.
Naye Ofisa Uchaguzi wa NEC Sada Kangeta, alisema kuwa tayari
wameshafanya uhakiki wa vifaa vya uchaguzi na wamejiridhisha kuwa vifaa vyote
vipo kama inavyopaswa na kwamba hatua itakayofuata ni usafirishaji wa vifaa
hivyo katika maeneo husika.
Pamoja na mambo mengine, aliwataka pia wapiga kura wote waliopo
katika maeneo husika, wagombea wa vyama vyote vya siasa na wadau wa siasa
kutokuwa na hofu juu ya vifaa hivyo kwa madai kuwa hakuna upungufu wowote
utakaojitokeza.
No comments:
Post a Comment