Tuesday, November 14, 2017

WANAOTOA KIBALI CHA KUSAFIRISHA KAHAWA MBINGA WALALAMIKIWA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

VIONGOZI waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuondoa urasimu kwenye masuala yanayohusiana na biashara ya zao la kahawa ili mfanyabiashara anayeuza kahawa yake mnadani Moshi aweze kuiuza kwa wakati uliopangwa.

Hayo yalisemwa na Meneja uzalishaji wa Kampuni ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Mbinga (MCCCO), Injinia Rabiel Ulomi wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu huku akielezea namna wafanyabiashara wa zao hilo wanavyopata vikwazo pale wanapohitaji kupata kibali cha kusafirishia kahawa.

“Ni muhimu jambo hili viongozi wetu wa ngazi ya halmashauri zetu wakaondoa urasimu wa mambo fulani fulani, hasa wakati wa kutoa kibali cha kusafirishia kahawa kwa sababu tu ya sahihi ya mtu mmoja hili ni lazima tuliseme wazi linaharibu biashara ya kahawa”, alisema Ulomi.

Pia alibainisha kuwa yeye binafsi hajaona jitihada za makusudi zinazofanyika katika kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa mkulima shambani hivyo alisisitiza kwamba halmashauri zinapaswa kumsaidia mkulima ili aweze kuongeza uzalishaji huo.

Ulomi alisema endapo mkulima ataongeza uzalishaji hata mapato ya halmashauri yataweza kuongezeka na fedha zitakazopatikana zitaweza kuhudumia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

 “Wakulima wazalishe kahawa yenye ubora unaoweza kufikia viwango vya kimataifa na pia nawashauri Watanzania wenzangu wawe na mazoea ya kunywa kahawa wanayozalisha wenyewe hususan kwa wanambinga ambao ndiyo wanazalisha zao hili kwa wingi”, alisema.

Alisema kahawa inayozalishwa na wakulima wa Mbinga ni ile yenye harufu na muonjo mzuri ambao unapendwa na watu wengi duniani kwa sababu uzalishaji wake ni wa milimani na imekuwa ikiandaliwa katika mazingira mazuri.

Awali alisema kuwa katika msimu huu wa mwaka 2017/2018 MCCCO wanatarajia kukoboa tani 8,000 ambapo mpaka sasa wameweza kufikia tani 7,400 na kwamba kiwanda kinaendelea kupokea kahawa kutoka kwa wakulima na wafanyabiashara mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji, wilaya ya Mbinga kahawa inayotegemewa kuzalishwa kwa kila msimu ni tani 12,000 ambapo kwa shughuli ya ukoboaji kwa kiwanda hicho zaidi ya asilimia 62 ya kahawa imepokelewa na kukobolewa licha ya wilaya hiyo kuwa na viwanda vitatu vya kukoboa zao hilo.

No comments: