Na Albano Midelo,
Songea.
IMEELEZWA kuwa Serikali hapa nchini,
imekubali kuwalipa fidia ya ardhi shilingi bilioni 3.3 wananchi wanaoishi
katika kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Aidha eneo ambalo hulipwa fidia ni
lile lenye ukubwa wa ekari 5,000 lililochukuliwa na Serikali katika mwaka wa
fedha wa 2008/2009 kwa ajili ya eneo maalum la Ukanda wa Uwekezaji Viwanda
(EPZA).
Hayo yalisemwa na Meya wa Manispaa
hiyo, Abdul Hassan Mshaweji wakati alipokuwa akitoa taarifa katika mkutano wa
baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea lililoketi mjini hapa.
Mshaweji aliliambia baraza hilo kuwa
Kamati maalum ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama
ilifanikiwa kwenda Dodoma kukutana na uongozi husika na hatimaye kuweza kufikia
muafaka wa kulipa fidia hiyo.
Alifafanua kuwa Serikali katika mwaka
huu wa fedha 2017/2018 italipa fidia ya shilingi bilioni 1.5 kwa wananchi hao
ili kupunguza deni hilo ambalo wananchi wamekuwa wakidai kwa muda mrefu.
Wananchi 1,181 wa kata ya
Mwengemshindo wanadai fidia ya shilingi bilioni 3.3 ambapo hadi sasa Serikali
imelipa shilingi bilioni mbili za fidia kwa wananchi hao.
Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya
madiwani wameiomba Serikali kulipa fidia hiyo haraka kwa kuwa wananchi
wamechoka kusubiri ambapo baadhi yao wamefariki dunia bila kupata haki yao.
Diwani wa kata ya Mwengemshindo,
Osmundi Kapinga alisema Serikali ilichukua ekari 5,000 za wananchi miaka kumi iliyopita
ambapo hadi sasa fedha za fidia ambazo zimelipwa ni shilingi bilioni mbili tu
kati ya fedha zaidi ya shilingi bilioni tano ambazo wanadai wananchi hao.
“Katika mkutano mkuu wa kata
uliofanyika hivi karibuni tumeazimia kuchukua ardhi yetu bila masharti yoyote
ili tuweze kuzalisha na kujenga nyumba kwa sababu wananchi wamekata tamaa na
kuchoshwa na ahadi ambazo hazitekelezeki kwa muda mrefu sasa”, alisema Kapinga.
Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Songea,
Yobo Mapunda alikiri kuwa madai hayo ni ya muda mrefu ndiyo maana wananchi
wamekata tamaa, hata hivyo alisema anaimani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuwa ni sikivu na itaweza kulipa kabla ya mwaka huu wa fedha haujakwisha.
No comments:
Post a Comment