Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKATI Rais Dokta John Pombe Magufuli
akisisitiza suala la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali hapa nchini,
hali hiyo imekuwa kinyume kwa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo
agizo hilo linaonesha kupuuzwa kutotekelezwa ipasavyo na sasa mji huo umeshamiri uchafu katika mitaa
yake na kuwa kero katika jamii.
Mara baada ya Rais Dokta Magufuli
kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana alianzisha Operesheni maalum ya
kufanya usafi ambayo imeendelea hadi sasa, kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi
kuwa ndiyo siku ya usafi kuanzia alfajiri hadi saa 5:00 asubuhi.
Katika uzinduzi huo Rais alifanya
usafi eneo la Feri jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu
walifanya eneo la Kariakoo huku viongozi wengine wakishirikiana na wananchi
kufanya usafi katika maeneo yao.
Hivyo basi pamoja na wananchi wa mji
huo kuchangishwa fedha mara kwa mara kwa ajili ya kufanyia utekelezaji wa kazi
hiyo lakini hakuna jitihada zinazo onesha kuzaa matunda.
Kufuatia hali hiyo, baraza la Madiwani
wa halmashauri hiyo ambalo limeketi hivi karibuni mjini hapa, limelalamikia
uongozi husika kwa kutochukua hatua za makusudi katika kuhamasisha jamii ili
iweze kushiriki kikamilifu kuondoa taka kwenye maeneo hayo.
Vilevila baraza hilo limeutaka uongozi
huo kuchukua hatua za haraka kuondoa taka zilizofurika kwenye maghuba yaliyopo
mjini hapa kwani imefikia hatua baadhi ya maghuba kutoa harufu kali na
kuhatarisha usalama wa afya za wananchi.
Grace Millinga ambaye ni diwani wa
viti maalum kata ya Mbinga mjini, alisema kuwa tatizo kubwa lipo kwa wataalamu
husika ambao wanasimamia utekelezaji wa jambo hilo ambapo hata madiwani hawajui
ni namna gani walivyopanga mkakati wa namna ya kuzoa taka hizo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti tunataka leo
hii watueleze hapa katika kikao hiki, wamejipangaje namna ya kuzoa zile taka
kwenye maghuba huu mji wetu ni mchafu”, alisema Millinga.
Naye diwani wa Mbinga mjini A, Aurelia
Ntani akizungumzia juu ya tatizo hilo ambalo limefikia hatua ya kuwa kero kwa jamii
aliongeza kuwa hata ghuba lililokuwa eneo la Soko kuu mjini hapa, ambako
vyakula vingi vimekuwa vikiuzwa hapo taka nyingi zimerundikana zikitoa harufu
kali huku inzi wakiwa wamezagaa na hakuna usafi unaofanyika.
Kwa upande wake baraza hilo la
Madiwani wa mji wa Mbinga lilipomtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji
huo, Robert Kadaso Mageni kutolea maelezo juu ya kero hiyo alikiri hali ya mji
kuwa mchafu na kueleza kuwa kuna mikakati ambayo inaendelea kufanyika katika
kupambana na hali hiyo.
“Suala la usafi hapa mjini ni kweli
maghuba ni machafu tumeshauri kuna vikundi vitakavyokuwa vinajishughulisha na masuala
ya usafi katika mji vitajipanga ili kuweza kuanza kutatua kero hii,
“Tunataka kwa wale ambao ni
wazalishaji wa taka, wazitunze taka wao wenyewe na halmashauri itakuwa inazipitia
na kwenda kuzimwaga katika eneo husika kwa ajili ya kuziteketeza”, alisema
Mageni.
Mageni alisema kuwa kwa kushirikiana
na watendaji waliopo katika kata husika utekelezaji huo utakuwa unafanyika
lakini pia kuna sheria mpya ambazo zinaandaliwa na sasa wamefikia hatua ya
mwisho ya kumaliza taratibu husika ili ziweze kuanza kufanya kazi ya kusimamia
na kudhibiti kero hiyo.
No comments:
Post a Comment