Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema akiwa katika mtaa wa Mwinyi mkuu moyo uliopo katika Manispaa ya Songea akihamasisha zoezi la kufanya usafi katika mitaa mbalimbali mjini hapa. |
Na Albano Midelo,
Songea.
MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Palolet Kamando Mgema
amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea mkoani humo kwa kushirikiana
na maafisa wake wa afya, kuwahimiza wananchi katika Manispaa hiyo waweze
kushiriki kikamilifu kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kufanya usafi katika
maeneo ya umma.
Aidha alisisitiza kuwa kwa yule mwananchi ambaye hatashiriki
katika siku hiyo maalum ya kufanya usafi achukuliwe hatua ikiwemo kutozwa faini
ya shilingi 50,000.
Mgema alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa katika mtaa wa
Mwinyi mkuu moyo uliopo katika kata ya Majengo mjini hapa, huku akishirikiana
na wananchi wa mtaa huo kufanya usafi wa Mazingira.
Alisema kuwa sheria ya usafi wa mazingira inawatia hatiani
wale wote waliosababisha kuwepo kwa uchafu katika eneo husika na wale
wanaokataa kufanya usafi adhabu yake ni faini ya shilingi 50,000.
Kadhalika aliwaagiza Watendaji wa mitaa waliopo katika
Manispaa ya Songea kuwaandika majina wananchi wanaoshiriki usafi huo kila Jumamosi
ya mwisho wa mwezi na kwamba kwa wale ambao hawashiriki watozwe faini na ofisi
yake ipelekewe taarifa haraka ni wangapi wamelipa fedha kutokana na kupigwa faini
ya kutoshiriki katika kufanya usafi wa mazingira.
Mgema amezitaka kaya zote zinazoishi katika mitaa 95 iliyopo
kwenye Manispaa hiyo kuchangia mchango wa usafi wa mazingira ambao ni shilingi
2,000 kila mwezi.
“Usafi wa mazingira ni jambo la lazima ili tuweze kukabiliana
na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu na malaria”,
alisisitiza.
Hata hivyo alisema katika nchi zilizoendelea hakuna watu
wanaougua magonjwa yanayotokana na uchafu kutokana na kuzingatia masuala ya
usafi na kwamba nchi hizo zinashangaa kuona kuna watu wanaugua na kufa kutokana
na magonjwa ya uchafu.
No comments:
Post a Comment