Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi. |
Dodoma.
SERIKALI imeanza kutoa hati za
kumiliki ardhi ndani ya kipindi cha siku 30 tangu kupokelewa kwa maombi tofauti
na awali ambapo mchakato wa kupata hati hizo ulichukua zaidi ya siku 90, ikiwa
ni matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa ili kuondoa changamoto
zinazoikabili sekta ya ardhi hapa nchini.
Akizungumza katika kipindi maalum cha
TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO), Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi alisema dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ni
kuhakikisha kwamba kila kipande cha ardhi kinapimwa na kumilikishwa.
“Tumejipanga vizuri na sasa taarifa
zote za ardhi zitakuwa katika mfumo wa kielektroniki utakaounganisha taarifa za
nchi nzima hivyo tutaweza kudhibiti vitendo vyote vilivyokuwa vikifanyika awali
kinyume na utaratibu na kuchochea kuongezeka kwa migogoro ya ardhi hapa nchini”,
alisisitiza Lukuvi.
Aliendelea kusema kuwa, hatua zinazochukuliwa
na Serikali hivi sasa ni pamoja na kutenga muda wa kuwasikiliza wananchi na
kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ikiwemo kudhulumiwa viwanja ambapo
Serikali imekuwa ikirudisha umiliki kwa wananchi husika pale inapojiridhisha
kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo husika.
Aliongeza kuwa mapato ya Serikali yameongezeka
kutoka milioni 46 hadi bilioni 100 kwa mwaka ikiwa ni kodi ya Ardhi na kwamba kuongezeka
kwa mapato hayo kumetokana na usimamizi madhubuti wa Serikali katika sekta ya
ardhi hapa nchini ili kuwapa wananchi wote fursa ya kutumia ardhi na kujiletea
maendeleo.
Vile vile alifafanua kuwa hatua
nyingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuanzisha Ofisi za Kanda
zitakazokuwa zikitekeleza majukumu yanayotekelezwa na wizara ikiwemo kutoa hati
ili kusogeza huduma kwa wananchi hasa wanyonge waliopo vijjini ambao mara
nyingi hushindwa kusafiri hadi makao makuu ya wizara kufuata huduma hizo.
Pia Lukuvi alibainisha kuwa Serikali
imenunua vifaa vya upimaji ardhi vitakavyotumika katika Ofisi za Kanda ili kuwawezesha
watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hali itakayosaidia sekta
hiyo kutoa mchango mkubwa katika kujenga uchumi.
“Hati za kimila elfu 46,000
zimeshatolewa kwa wananchi ili kuwawezesha kuwa na miliki salama ambazo
zitachochea maendeleo katika maeneo yao kwani zinaongeza thamani ya ardhi ya
eneo husika, vile vile maeneo ya makazi zaidi ya 200,000 yametambuliwa na kurasimishwa”,
alisisitiza Lukuvi.
Aidha Lukuvi aliwaasa wamiliki wa
mashamba makubwa kuyaendeleza vinginevyo Serikali itayatwaa na kuyamilikisha
kwa wananchi ili wayatumie kwa shughuli za uzalishaji ambapo kwa sasa mashamba
makubwa zaidi ya 150 yamefutiwa umiliki na kurudishwa kwa wananchi.
Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo
ya makazi ni moja ya Sekta muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda na imekuwa
ikichukua hatua mahususi katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya
Ardhi.
Hatua hizo zinajumuisha ujenzi wa
Kanzi Data ya taarifa za ardhi kwa nchi nzima na pia kuunganisha mifumo yake na
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo
katika kujenga uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment