Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma Palolet Mgema amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo,
kusimamia ipasavyo bei ya pembejeo za kilimo ili kuepusha ulaghai unaoweza kufanywa
na baadhi ya mawakala ambao sio waaminifu waliopewa dhamana na Serikali
kusambaza pembejeo hizo kwa wakulima katika kuelekea msimu huu wa kilimo.
Palolet Mgema. |
Mgema alitoa agizo hilo mwishoni mwa
wiki alipokuwa akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya wilaya ya Madaba huku akisisitiza kuwa wanaowajibu pia wa
kusimamia hilo kuhakikisha mkulima anauziwa kwa bei iliyopangwa.
Alisisitiza kuwa endapo viongozi hao
watapuuza na kuwaachia mawakala wafanye wanavyotaka, kuna uwezekano mkubwa kwa
wakulima kuuziwa kwa gharama kubwa hatimaye kushindwa kumudu gharama husika na kusababisha
baadhi yao kutozalisha mazao yao shambani.
Katika hatua nyingine, Mgema alisema
kuwa Ng’ombe ambao wamezuiliwa kuingia katika wilaya ya Songea wanaotoka maeneo
mengine nje ya wilaya hiyo, ni wale wanaoingizwa kwa ajili ya kutafuta malisho
na ufugaji hivyo Serikali imeruhusu kuingizwa kwa ng’ombe wanaoletwa kwa ajili
ya wananchi kupata nyama tu na sio vinginevyo.
Alisema tatizo kubwa la uingizaji wa
mifugo kiholela katika wilaya ya Songea hasa kwa halmashauri ya wilaya ya
Madaba limechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya watumishi waliopo kwenye halmashauri
hizo ambao wamepewa dhamana ya kusimamia hilo kujihusisha na vitendo vya rushwa
huku baadhi yao wakiruhusu wafugaji kuingiza mifugo yao bila kuzingatia sheria
na taratibu zilizowekwa.
Hata hivyo aliwataka viongozi hao
watekeleze maagizo wanayopewa na Serikali ipasavyo na sio kuyapuuza kwani
atakayefanya tofauti kinyume na taratibu zilizowekwa hatua kali za kisheria
zitachukuliwa ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment