Thursday, November 16, 2017

NFRA MANISPAA SONGEA KUNUNUA TANI 400 ZA MAHINDI


Na Mwandishi wetu,       
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepangiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika msimu huu mkoani humo kununua mahindi tani 400.

Afisa kilimo wa Manispaa ya Songea, Mushoborozi Christian amefafanua kuwa halmashauri hiyo imepokea barua toka kwa wakala huyo ambayo inatoa maelekezo ya ununuzi wa mahindi hayo kwa awamu ya tatu msimu wa mwaka 2017/2018.

Alisema katika Manispaa ya Songea kata saba tu, kati ya kata 21 NFRA inaruhusiwa kununua mahindi katika vituo husika ambapo wananchi wanatakiwa kuyapeleka haraka kwa ajili ya kuuza.

Mushoborozi anazitaja kata ambazo zinahusika katika ununuzi wa mazao hayo kuwa ni Lilambo ambayo imepangiwa kununua tani 100, Subira 100, Mjimwema 40, Ruhuwiko 40, Mshangano 40, Matogoro 30 na Ndilimalitembo tani 30 hivyo kufanya jumla ya tani 400.

Kadhalika mtaalam huyo wa kilimo aliwaasa wananchi wote wanaouza mazao hayo, kuhakikisha kwamba wanapopeleka kuyauza yasiwe na uchafu ili kuondoa usumbufu na kwamba wananchi wanatakiwa kuuza mahindi kulingana na mgawo wa ununuzi kwa kila kata husika.

“Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya kata kutofikia malengo ya Serikali ya kuuza mahindi NFRA, katika awamu hii Afisa mtendaji wa kata atakayeshindwa kuhamasisha wakulima wake kuuza mahindi atawajibishwa’’, alisisitiza.

Alisema kuwa mkulima anaruhusiwa kuuza tani moja tu ya mahindi kwa Wakala huyo ambapo bei ya kilo moja ni shilingi 500 na kwamba zoezi hilo la kupeleka mahindi litakamilika Novemba 17 mwaka huu.

No comments: