Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
PONGEZI zimetolewa na baadhi ya
Wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kwa
jitihada za kuchangia maendeleo katika mji huo zinazofanywa na aliyekuwa Mbunge
wao, Gaudence Kayombo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema kuwa Kayombo, wanampongeza kwa
kutafuta Wafadhili kutoka Ubalozi wa Korea kusini na hivi sasa wanatarajia
kuanza kujenga Kituo cha elimu katika mtaa wa Lulambo kata ya Matarawe mjini
hapa.
“Ushirikiano huu anaoufanya wa
kutujali na kutukumbuka sisi wananchi wake ni ishara tosha inayothibitisha ni
mtu ambaye anafaa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo yetu, tunachoomba
kituo hiki kijengwe kwa wakati ili kuweza kuanza kutoa huduma kwa jamii”,
walisema.
Vilevile walieleza kuwa umefika
wakati sasa mji wa Mbinga unapaswa kuwa na maendeleo yanayokua kwa kasi,
hususan katika sekta ya elimu ambayo ndiyo msingi mkuu wa kukuza vipaji vya
aina mbalimbali kwa vijana na faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Awali akizungumza katika sherehe za
uzinduzi wa eneo la ujenzi wa kituo hicho zilizofanyika Novemba 15 mwaka huu kwenye
kata hiyo Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru
alipongeza hatua hiyo na kueleza kuwa ujenzi huo unapaswa kuungwa mkono kwa
asilimia kubwa ili mji huo uweze kuwa na maendeleo.
“Tukio hili ni la kimaendeleo tunajua
Mbinga tumekwama katika shughuli nyingi sana za maendeleo ujenzi wa chuo hiki
utazalisha mafunzo mengi ya ualimu na sekta ya afya”, alisema Ndunguru.
Pamoja na mambo mengine, kukamilika
kwa ujenzi wa kituo hicho ambacho ni chuo cha mafunzo katika sekta ya elimu na
afya utagharimu dola za Kimarekani milioni 150.
No comments:
Post a Comment