Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
MADIWANI waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa wahakikishe kwamba wanasimamia
ipasavyo maendeleo ya wananchi ili mwisho wa siku wananchi waliowachagua waendelee
kuwa na imani nao.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa huo, Christine Mndeme wakati
alipokuwa juzi katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa huku akiwataka
Madiwani hao katika kata zao kufanya mikutano na wananchi ambayo inalenga
kujadili masuala ya kimaendeleo.
“Ndugu zangu maana mkizembea kufanya hivi siku ya mwisho wa
utawala wenu kule katani waliotuajiri hawatatuelewa tena”, alisema Mndeme.
Vilevile aliwataka kuwa na mahusiano mazuri kati yao na watendaji
wa halmashauri lakini pale wanapoona mambo ya kimaendeleo hayaendi vizuri
wanapaswa kuchukua hatua haraka kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.
Kwa upande wa kukuza uchumi alisisitiza ufanyike uhamasishaji
wa kutafuta wawekezaji waliopo ndani na nje ya wilaya, kwa kuwapatia fursa ya
kujenga viwanda ambavyo vitasaidia kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na
hatimaye wananchi waweze kuondokana na umaskini.
“Tunapokuwa na viwanda vya usindikaji tutaweza kukuza uchumi
wa wilaya yetu, tuitangaze Mbinga ili watu waje wawekeze hapa tusiweke
urasimu”, alisema.
Mndeme amewataka pia Wakurugenzi watendaji waliopo kwenye
halmashauri hizo waondoe urasimu pale wawekezaji hao wanapojitokeza na kutaka
kuwekeza kwa namna mbalimbali ikiwemo ujenzi huo wa viwanda.
Akizungumza mara baada ya Mndeme kutoa nasaha zake naye Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose Nchimbi alisema kuwa watazingatia
maagizo na maelekezo aliyoyatoa Mkuu huyo wa mkoa ili kuweza kufikia malengo
husika kwa manufaa ya wananchi.
Nchimbi alimuomba pia Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma atatue
tatizo la upungufu wa walimu kwa shule za msingi na sekondari ambalo
linaikabili wilaya ya Mbinga kwa muda mrefu na ndiyo kikwazo kikubwa
kinachoifanya wilaya ishindwe kusonga mbele katika sekta ya elimu ambapo naye
alisema atalifanyia kazi ili kuweza kuondokana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment