Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo akizungumza leo na Waandishi wa habari mjini Dodoma. |
Na Mwandishi wetu,
WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameitaka mikoa yote nchini, kuanza mapema
maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018 kufuatia uwepo
wa ongezerko la ufaulu.
Jafo alitoa kauli hiyo leo mjini Dodoma, wakati akizungumza na
Waandishi wa habari, juu ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na
kidato cha kwanza mwaka mwakani.
“Wakuu wa mikoa hakikisheni miundombinu iliyopo inatosha
katika mikoa yenu ili watoto wote waliofaulu wapate nafasi ya kujiunga na
kidato cha kwanza hapo Januari mwaka 2018”, alisisitiza.
Ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Njombe,
Tanga, Morogoro, Lindi, Rukwa, Pwani, Mtwara na Songwe kuwa ndiyo yenye idadi
kubwa na kwamba maandalizi ya madarasa, vyoo na madawati yatahitajika kwa
kiwango kikubwa.
Kadhalika amewataka Makatibu tawala wa mikoa, kusimamia zoezi
la uchaguzi wa wanafunzi tarajiwa wa kidato cha kwanza ili ifikapo Disemba 8
mwaka huu wawe wamekwisha tangaza.
Pia Jafo ameagiza kufanyika uchambuzi ili kubaini sababu
zilizopelekea watahiniwa zaidi ya asilimia moja kutofanya mitihani katika mikoa
ya Geita, Katavi, Mara, Rukwa, Songwe, Dodoma na Manyara kwa lengo la kuondoa
mdondoko wa wanafunzi kutoka ngazi moja hadi nyingine.
Vilevile amezitaka halmashauri zilizopata ufaulu chini ya
asilimia hamsini kujiwekea mikakati ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi, ambapo halmashauri
hizo ni pamoja na Mkalama, Meatu na Simanjiro.
Matokeo ya darasa la saba yalitangazwa rasmi hivi karibuni
ambapo jumla ya watahiniwa wapatao 662,035 walifaulu kwa kupata daraja A, B na
C, ikiwa ni sawa na asilimia 72.76 ya watahiniwa wote.
Ofisi ya Rais TAMISEMI ndiyo yenye dhamana na usimamizi wa
elimu ya awali, msingi na sekondari imechukua hatua za makusudi, kupunguza au
kuondoa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kutopangiwa shule na
kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
No comments:
Post a Comment