Na Dustan Ndunguru,
DOKTA John Pombe Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, tangu aingie madarakani mwaka 2015 amekuwa akiwaasa Watanzania
kuwa wazalendo kwa nchi yao ambapo hata wateule wake amewataka kufuata nyendo
za serikali yake anayo iongoza, ili kwa pamoja waweze kuleta mabadiliko ya
kweli ambayo wananchi wamekuwa wakiyalilia.
Ni ukweli usiopingika kwamba Rais Magufuli siku zote amekuwa
akipambana na mafisadi ambao miaka mingi wamekuwa na kawaida ya kuiba
rasilimali za Watanzania, jambo ambalo linawafanya wananchi walio wengi
wakumbwe na changamoto nyingi ikiwemo ubovu wa barabara, ukosefu wa madawa
kwenye zahanati na hospitali na mengine mengi huku wale ambao waliamua kwa
makusudi kujilimbikizia mali wakiishi kama wafalme bila kuwajali wengine wenye
shida.
Serikali ya awamu ya tano imeonesha dhamira ya dhati katika kuwatumikia
wananchi wake ikiwemo kusimamia kikamilifu rasilimali zilizopo kama vile
madini.
Hali hiyo imewafanya wananchi kujenga imani kwa
Serikali yao waliyoichagua ukizingatia kwamba, matunda ambayo wamekuwa
wakiyakosa kwa miaka mingi wameanza kuyaona kwa njia mbalimbali.
Lakini yatupasa kutambua kuwa Rais Magufuli siku zote hapendi
na amekuwa akichukizwa kuona pale mteule wake akikiuka maagizo aliyopewa ambayo amekuwa
akiyatoa kila mara hasa katika kusimamia rasilimali za taifa hili ambazo kama
inavyofahamika, wakati mwingine zimekuwa zikitumika vibaya na baadhi ya watu wachache ambao
wamekuwa na tabia mbaya ya kutaka kujilimbikizia mali za wananchi na hatimaye
mwisho wa siku anemeeke yeye binafsi huku mwananchi wa kawaida akiendelea
kubaki kuwa maskini.
Ikumbukwe kuwa wakati Wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa,
majiji na wilaya wanaapishwa walisisitizwa kusimamia mapato ya ndani katika
halmashauri zao ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwahudumia
wananchi ipasavyo.
Pamoja na kuapishwa, Wakurugenzi hao walikula kiapo cha
maadili ya utumishi wa umma pamoja na ahadi ya kuwa waaminifu na wazalendo kwa
nchi yao ambapo baada ya hapo kila mmoja wao alikwenda kwenye eneo lake la kazi
tayari kutekeleza majukumu yake ya kazi aliyopewa.
Wakurugenzi hawa wanaowajibu wa kusimamia mikataba iliyopo na
ile ambayo halmashauri inaingia na Wazabuni walioshinda tenda mbalimbali, ikiwa
ni pamoja na kuzingatia masharti ya mikataba hiyo wakati wa utekelezaji wake
huku wakitakiwa kuwa wazi katika uwajibikaji wake kwa mamlaka husika waliyonayo
kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Binafsi natambua kuwa Mkurugenzi mtendaji katika halmashauri yoyote
ile ndiye anayebeba bendera ya maendeleo na dhamana ya kusimamia sekta zote ndani ya
halmashauri ikiwemo afya, kilimo, elimu, maji, uvuvi ambazo zikisimamiwa vizuri
huwaletea maisha bora Watanzania.
Haya yote yanawezekana endapo tu mteule huyo wa Rais atakuwa
makini kutekeleza majukumu yake ya kazi aliyopewa, ikiwemo kutembelea maeneo yake
katika halmashauri na kujionea changamoto zinazowakabili wananchi wake ikiwemo
kuzitafutia ufumbuzi wa haraka badala ya kukaa muda mwingi ofisini.
Kana kwamba haitoshi Mkurugenzi huyo anaowajibu wa kufuatilia
na kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo ndani ya halmashauri yake kwa
kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali ili kuweza kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Robert Kadaso Mageni. |
Oktoba 20 mwaka huu kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo
kilifanyika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga
mkoani Ruvuma, ambapo Wajumbe wa Kamati maalum ya kuchunguza ubadhirifu wa
fedha za msitu wa Mbambi unaomilikiwa na mji huo siku hiyo ya kikao walikuwa wakiwasilisha
taarifa za uvunaji wa msitu huo ambao kazi hiyo ya uvunaji ilifanyika mapema
kuanzia mwezi Januari mwaka huu.
Baada ya taarifa ya kamati kutolewa ilionesha wazi kuwa Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya mji huo, Robert Kadaso Mageni alikuwa mmoja kati ya
watendaji ambao walishiriki katika kuhujumu mapato ya msitu huo na hivyo
kuingiza hasara ndani ya halmashauri jambo ambalo mpaka sasa limeweza kuzua
gumzo kubwa na kuwakatisha tamaa wananchi wa kata ya Matarawe na maeneo mengine kuzunguka halmashauri hiyo ambao kwa miaka 30 wamefanya kazi kubwa ya kushiriki katika kuutunza msitu huo.
Katika taarifa iliyosomwa na Katibu wa kamati hiyo maalum
iliyoundwa na baraza hilo la Madiwani Julai 27 mwaka huu, limetoa
mapendekezo yake ya kumkataa Mkurugenzi huyo kwamba hawataki kufanya naye kazi
tena, wakimtuhumu ametafuna fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu
wa Mbambi uliopo mjini hapa ambao ni mali ya halmashauri ya mji huo.
Imeelezwa kuwa Mageni anaingia katika kashfa pia ya kulipotosha baraza hilo katika
kikao walichoketi mwezi Novemba 2 hadi 3 mwaka jana na kutoa taarifa za uongo
kwamba msitu huo una jumla ya miti 5,4040 ambayo inafaa kupasuliwa mbao wakati
ukweli ni kwamba msitu ulikuwa na miti 8,470.
Kufuatia taarifa hizo ambazo hazikuwa sahihi wakati anazitoa
kwenye baraza hilo juu ya uvunaji wa msitu huo, hali hiyo imesababisha
halmashauri kupata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800 wakati huo huku halmashauri
anayoiongoza ikiendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinalenga mahitaji
ya wananchi ikiwemo hospitali ya wilaya hiyo kukosa hata gari la kubebea
wagonjwa, majokofu ya kuhifadhia maiti pamoja na chumba bora cha kufanyia upasuaji.
Baada ya baraza hilo kutoa mapendekezo hayo ya kumkataa,
walimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kufikisha kilio chao kwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ili aweze
kuchukua hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya mtumishi huyo.
Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa tuhuma hizo mbele ya
baraza hilo ambalo lilihudhuriwa na mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga wakiwemo na
Wajumbe wa kamati yake ya ulinzi na usalama, katibu wa kamati ya kuchunguza
tuhuma hizo Benedict Ngwenya ambaye ni diwani wa kata ya Mpepai alisema kuwa
Mkurugenzi, Mageni ameshirikiana na watendaji wake wa halmashauri ya mji huo
kuhujumu mapato hayo.
Ngwenya anafafanua kuwa ufisadi huo uliofanyika, Mkurugenzi
ameshirikiana na baadhi ya watendaji wake wa halmashauri ambao waliteuliwa kwa
ajili ya kufanya kazi ya kusimamia uvunaji wa msitu wa Mbambi ambao watendaji
hao aliwataja kuwa ni Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera na
mlinzi mkuu Efreim Kawonga.
“Kwa msingi huu kamati ilibaini mbao nyingi ziliibwa kwa
kisingizio kwamba zimekwenda kwenye shughuli ya mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa
wakati sio kweli na hata fedha zilizotokana na uvunaji huo tumefuatilia kwenye
akaunti husika hakuna fedha iliyoingizwa”, alisema Ngwenya.
Anafafanua kuwa thamani hiyo halisi na ubadhirifu uliofanyika
katika msitu wa Mbambi waliweza kuipata baada ya kamati hiyo kufanya uchunguzi
wa kina kwa kuwatumia wataalamu waliobobea katika masuala ya uvunaji wa misitu
ambao walitoka nje ya halmashauri ya mji wa Mbinga.
“Mapendekezo ya awali aliyoyaleta Mkurugenzi huyu Novemba 12
mwaka 2016 katika baraza lililopita la Madiwani alituambia kwamba msitu huu
baada ya mavuno zingepatikana shilingi milioni 325,000,000 lakini hadi leo hii
tunaambiwa mapato yaliyopatikana ni shilingi milioni 130,000,000 tu jamani
kweli hata katika mtazamo wa kawaida jambo hili linaweza kuingia akilini ?”,
alihoji Ngwenya.
Anaeleza kuwa hasara hiyo iliyopata halmashauri kutokana na
uzembe uliofanyika na watendaji hao ambao wamepewa dhamana na Serikali
kusimamia shughuli za maendeleo na mali za umma, wanapaswa kuchukuliwa hatua za
kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia
kama hiyo.
Ngwenya anaongeza kuwa hasara hiyo imesababishwa pia kutokana
na taratibu husika zilizowekwa wakati wa kupasua mbao katika msitu huo,
hazikufuatwa kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo kwamba hata Mkurugenzi huyo
amekiuka baadhi ya sheria ambazo zinakataza suala la Serikali kufanya biashara
ya kuuza mbao badala yake ilitakiwa kuuza miti iliyopo kwenye msitu huo baada
ya upembuzi yakinifu kufanyika.
Anabainisha kwamba Mkurugenzi, Mageni alipaswa pia kulieleza
bayana baraza hilo la Madiwani kwamba Serikali haifanyi biashara ya mbao kwa
mujibu wa sheria hiyo lakini alilipotosha na hakuweza kutoa ufafanua wowote
ikidaiwa kuwa alikuwa na lengo la kutaka kujinufaisha yeye binafsi kupitia
mauzo ya mbao hizo.
“Kama tungefuata taratibu za Serikali hasara hii tungeweza
kukabiliana nayo lakini mtaalamu wa misitu, Hyera alishindwa hata kumshauri
Mkurugenzi wake juu ya taratibu za zabuni za uvunaji wa msitu huu, badala yake
wametumia mbinu za ujanja kumtafuta mzabuni ambaye wanamjua wao bila kufuata
taratibu husika ambapo kamati hii maalum ilipofanya uchunguzi wa kina tumebaini
zabuni ya kuvuna msitu ule na mikataba yake haikufuata taratibu”, anasema.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Ndunguru
Kipwele akizungumza katika kikao hicho anasema kuwa anaipongeza kamati kwa kazi
nzuri iliyofanya ya kuchunguza jambo hilo na kueleza kuwa baraza linaafiki juu
ya mapendekezo yaliyotolewa kwa kuiomba Serikali ichukue hatua kali za
kinidhamu dhidi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kwa kuwa mamlaka
iliyomteua ni ya Rais wa nchi.
Kadhalika alisema baraza limependekeza pia mtaalamu wake wa
misitu, Hyera na mlinzi mkuu, Kawonga wafukuzwe kazi na kufikishwa kwenye
vyombo vya kisheria.
“Niwaombe watendaji wetu kwa dhati wote kwa pamoja tumsaidie
Rais wetu maana ana dhamira nzuri sana kwa watanzania lakini inakuwa pia nia
aibu kwa mteule wake kutenda hayo ambayo yamefanyika na kuikosesha halmashauri
mapato yake”, anasema Kipwele.
Alipohojiwa na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo, Mageni anasema kuwa yeye hawezi kuzungumzia jambo lolote hivi
sasa juu ya tuhuma hizo kama ni za kweli au la.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye aliipongeza
kamati hiyo ya uchunguzi wa msitu wa Mbambi huku akieleza kuwa, “taarifa hii
waliyoitoa hapa ni ya kweli kabisa kwa hiyo mimi niwapongeze sana na sisi
kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya baada ya kutoka hapa tunayo ya kufanya”,
anasema Nshenye.
Kwa upande wake Hamis Nanyanje ambaye ni mkazi wa kata ya
Matarawe ambaye pia alihudhuria kikao hicho cha baraza la madiwani pamoja na
kutoa pongezi kwa madiwani hao alisema akiwa mwananchi wa kata hiyo hakutegemea
kama bado kuna baadhi ya watumishi hapa nchini, ambao hawana uzalendo wa kweli
na wanaendekeza vitendo vya kutumia mali za umma kwa manufaa yao binafsi.
Nanyanje anaeleza kuwa jambo pekee lililopo hivi sasa ni kwa
wananchi na viongozi kushirikiana kuendelea kuwaumbua wale wote ambao
wataonekana kwenda kinyume na maagizo yanayotolewa na Rais Magufuli ya kuwataka
Watanzania kutanguliza uzalendo kwa nchi yao na sio vinginevyo.
Naye Emmanuel Mapunda mkazi wa Mbinga mjini anasema
kwa hayo yaliyotokea katika msitu wa Mbambi ni ushahidi tosha kuwa bado wapo
watendaji wachache katika halmashauri, ambao wanamawazo ya kutumia vibaya mali
za umma kwa kujinufaisha wao binafsi huku wananchi wakiendelea kuumia kwa
kukosa huduma muhimu ambazo walipaswa kuzipata kutokana na mapato yao ya ndani.
Kwa msingi huo hayo ambayo yamejitokeza katika halmashauri ya
mji wa Mbinga ya kuvuna msitu ambao wananchi wamekuwa wadau wazuri kwa kipindi
cha miaka 30 kuutunza, na kwamba baada ya uvunaji wamejitokeza watu wachache
kutumia vibaya madaraka yao kwa kuhujumu mapato ya msitu huo ni wakati sasa hatua
stahiki dhidi yao zichukuliwe ili iweze kuwa fundisho kwa viongozi wengine na
sio vinginevyo.
Ni dhahiri kuwa mapato ya msitu huo yangeweza kusaidia
kuwaondolea adha wananchi wa wilaya hiyo na majirani zao kwa kununua gari la
kubebea wagonjwa na kutatua kero nyingine.
Kutokana na matumizi haya mabaya ya fedha hizo tayari ile
asilimia 10 ambayo hata wananchi walipaswa kupewa kupitia vikundi vya vijana na
wanawake sote tunatambua imepotea, ambao makundi hayo yataendelea kuumia kwa
kukosa fedha ambazo zingeweza kuwasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali.
Sasa Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga mnapaswa
kuendelea kusimamia na kufuatilia kikamilifu hata fedha zinazotolewa na Serikali
kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ndani ya halmashauri yenu, ili kuweza kuona kama kweli zinafanya kazi
ile ambayo imepangwa na kwa viwango vinavyokubalika.
Hata hivyo nashauri kuwa tunapobaini kuna ubadhirifu au
matumizi yasiyo sahihi ya fedha hizo, wasisite kuchukua hatua stahiki kama
walivyofanya kwenye msitu huu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe halmashauri ya mji huo.
No comments:
Post a Comment