Saturday, November 4, 2017

MTOTO ANAYESOMA SHULE YA MSINGI NAIKESI NAMTUMBO AOMBA MSAADA WA MATIBABU

Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

MTOTO Shaziry Athuman (12) ambaye ni mwanafunzi anayesoma darasa la nne shule ya msingi Naikesi iliyopo katika kata ya Kitanda wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, anaomba msaada wa fedha za kugharimia matibabu yake kutokana na kusumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa moyo kuwa mkubwa.
Mtoto Shaziry Athuman.

Aidha kufuatia mtoto huyo kukabiliwa na ugonjwa huo, amekuwa akisumbuliwa pia na tatizo la kuvimba miguu, hali ambayo imekuwa ikisababisha kushindwa kuhudhuria masomo yake ipasavyo darasani.

Baba mzazi, Athuman Amani alisema kuwa licha ya kufanya jitihada ya kumpeleka mtoto wake katika hospitali zilizopo ndani ya mkoa huo hali ya mtoto inazidi kuwa mbaya na yeye kutokana na kukosa fedha anashindwa kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

“Ninawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie kunichangia fedha ili niweze kumtibu mwanangu, hivi sasa sina uwezo wa kumpeleka hospitali kubwa ambazo angeweza kupata matibabu”, alisema.

Kwa upande wake akizungumzia juu ya tatizo la mtoto Shaziry, Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo Alkwin Ndimbo alithibitisha kupokea taarifa za mtoto huyo na kueleza kuwa kuna kila sababu kwa Watanzania wenye uwezo na mapenzi mema, wamsaidie mtoto huyo kwa kumchangia fedha ili aweze kupatiwa matibabu kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo wa kifedha.


Hata hivyo kwa Watanzania wenye moyo wa kuweza kumsaidia mtoto huyo wanaweza kuwasiliana na mzazi wake kupitia simu namba, 062 9629872.

No comments: