Na Mwandishi wetu,
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa wadaiwa sugu ambao
hawafuati taratibu za kulipa madeni wanayodaiwa na Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) watapelekwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Hayo yalisemwa na Waziri huyo alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi makao makuu ya Ofisi za TTCL jijini Dar es Salaam,
akizungumza na Menejimenti ya kampuni hiyo.
Alisema kuwa wale wanaodaiwa ambao hawafuati taratibu za kulipa madeni hayo wanatakiwa wapelekwe Mahakamani kwani
wamekuwa wakiendelea kutumia huduma za kampuni hiyo huku wakijua kuwa ni
wadaiwa sugu.
Mhandisi Nditiye amesifia huduma ya
Conference Video Call inayotolewa na TTCL akieleza kuwa husaidia kupunguza
gharama kwa Serikali na kwamba huruhusu watu kufanya mikutano kupitia njia ya
mawasiliano na sio kukutana kama ilivyokuwa hapo awali.
“Huduma hii ya Conference Video Call
itasaidia kupunguza gharama kwa Serikali ambapo awali ilikuwa unatakiwa
kuwakusanya viongozi wote kuja katika mkutano, ila kwa huduma hii unaweza
kuzungumza nao wakiwa huko huko waliko”, alisema.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni
ya simu Tanzania, Waziri Kindamba alielezea namna kampuni yao ilivyoweza kukusanya
deni la shilingi bilioni 6.8 kwa kipindi cha miezi mitatu kutoka kwa wadaiwa hao
huku akifafanua namna mfumo huo wa Conference Video Call unavyoweza kufanya
kazi.
Waziri Kindamba aliongeza kuwa hivi
sasa TTCL inatekeleza mpango mkakati wa mageuzi ya kibiashara ikiwemo mabadiliko
ya kuwa kiongozi wa huduma za mawasiliano na TEHAMA katika soko la Tanzania.
Alisema kuwa wanayo matumaini kuwa
mchakato wa kupata sheria mpya ya kampuni hiyo kuja kuwa Shirika la Mawasiliano
iliyopitishwa Bungeni wiki iliyopita itakuwa ndiyo kichocheo cha kukua kwa
maendeleo ndani ya kampuni.
Hata hivyo kampuni ya TTCL imeweza
kukusanya takribani shilingi bilioni 6.8 za madeni ndani ya miezi mitatu kwa
wadaiwa sugu ambapo awali deni lilikuwa ni shilingi bilioni 10.7.
No comments:
Post a Comment