Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Novemba 23 mwaka huu anatarajia kuwasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya
kikazi ya siku tatu na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya
siasa na Serikali katika uwanja wa ndege uliopo Ruhuwiko mjini Songea.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme
akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari Ofisini kwake alisema kuwa
Waziri Mkuu huyo anatarajia kuwasili katika uwanja huo mjini hapa majira ya saa
saba kamili mchana.
Alisema kuwa mara baada ya kuwasili atapokea
taarifa ya maendeleo ya mkoa huo na ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa
ndege mjini Songea na baada ya hapo ataelekea wilayani Namtumbo ambapo
atafungua ghala la MIVARF, kuongea na madiwani, watumishi wa umma na wananchi
wa wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara.
Mndeme alifafanua kuwa atakapokuwa wilayani
humo, Novemba 24 mwaka huu Majaliwa ataendelea na ziara yake atasalimiana na
wananchi wa kijiji cha Mchomoro na kisha kuelekea wilayani Tunduru ambapo
atafanya mkutano wa hadhara, kijiji cha Rahaleo na kusalimiana na
wananchi wa kijiji cha Milonde kisha kuelekea Tunduru mjini.
Atakapokuwa wilayani Tunduru
atatembelea kituo cha afya Nakayaya, ghala la kuhifadhia korosho na kupokea
taarifa ya Chama kikuu cha ushirika (TAMCU) na kuzungumza na wananchi wa
wilaya hiyo katika uwanja wa michezo wilayani humo.
Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wananchi
kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo yote ambayo Waziri Mkuu atapita pamoja na
kuhutubia mikutano ya hadhara, ili waweze kupata fursa nzuri ya kumsikiliza na
kupokea maelekezo atakayotoa hususan katika shughuli za utekelezaji wa
maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment