Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa ushirikiano uliopo
kati ya Korea kusini na Tanzania, utaendelea kuimarishwa katika kusaidia kukuza
maendeleo ya wananchi hapa nchini, hususan katika kuboresha sekta ya elimu na
afya.
Aidha wananchi wa Wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, wameombwa kuzingatia hilo ili viongozi wa ubalozi wa Korea kusini
waweze kufanikiwa hatua ya kuboresha sekta hizo wilayani humo kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na baadaye.
Song, Geum – Young ambaye ni Balozi
wa nchi hiyo hapa Tanzania alisema hayo jana wakati alipokuwa kwenye sherehe ya
uzinduzi wa shughuli ya ujenzi wa Kituo cha elimu zilizofanyika katika mtaa wa
Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa.
“Ushirikiano wetu tulionao
tutaendelea kusaidia Watanzania na wanambinga kwa ujumla, lakini pia
tutahakikisha Korea kusini na Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye urafiki
mzuri”, alisema Song, Geum – Young.
Balozi huyo aliongeza kuwa kukamilika
kwa ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa chuo cha mafunzo ya sekta ya elimu
na afya kutaweza kuinufaisha pia jamii ya kutoka maeneo mbalimbali nje ya
wilaya hiyo.
Alifafanua kuwa ujenzi huo utaanza
mapema kuanzia sasa na kwamba utagharimu dola za Kimarekani milioni 150.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya
Mbinga, Cosmas Nshenye naye akizungumza katika sherehe hizo za uzinduzi
aliushukuru Ubalozi huo wa Korea kusini kwa moyo walionao katika kushirikiana
na wanambinga kuleta maendeleo hayo.
“Mimi kwa niaba ya wananchi wangu
nichukue nafasi hii kuwakaribisha nasema karibuni sana, Ofisi yangu itatoa
ushirikiano mkubwa kwenu kwa jambo lolote mtakalohitaji kupata ushirikiano
kutoka kwangu”, alisema.
Nshenye alieleza kuwa huduma
zitakazotolewa hapo wananchi wa wilaya hiyo wanapaswa kuzipokea kwa mikono
miwili kwani wataweza kupata fursa ya kuweza kukuza ajira na kujenga mahusiano
mazuri kati yao na wananchi wa Korea kusini.
Pia alisisitiza kuwa eneo hilo ambalo
ujenzi unafanyika lisiingiliwe ovyo na wananchi badala yake waendelee kutoa
ushirikiano kwa shughuli zitakazofanyika hapo kwa faida ya wananchi wote.
No comments:
Post a Comment