Gari aina ya Noah linalodaiwa kuteketea kwa moto eneo la Peramiho wilayani Songea baada ya fumanizi. |
Na Albano Midelo,
Songea.
GARI aina ya Noah limeteketea kwa moto katika eneo la
Peramiho wilayani Songea mkoa wa Ruvuma.
Taarifa za awali za mashuhuda waliohojiwa katika eneo la
tukio walidai kuwa gari hilo liliteketezwa, kutokana na sababu za fumanizi la
mke wa mtu ambaye inadaiwa kuwa mwenye mume aliamua kuteketeza gari hilo.
Uchunguzi umebaini kwamba ubavuni mwa gari hilo ambalo
limeteketea yameandikwa maneno kwa rangi nyeusi, kuwa mke wa mtu ni sumu ambapo
akinamama wanne waliokutwa katika eneo hilo walidai kuwa tukio hilo
lilisababishwa na fumanizi.
Mashuhuda wengine waliohojiwa walidai kuwa gari hilo
liliteketea kwa sababu ya hitilafu katika injini ya gari hali iliyosababisha
gari kuwaka moto na kuteketea.
Bado haijafahamika madhara ambayo wameyapata watu waliokuwemo
ndani ya gari hilo iwapo walitoka salama au wamepata majeraha katika tukio
hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy
amethibitisha kutokea kwa tukio la gari hilo kuteketea moto katika eneo la
Peramiho ambapo amesema tukio hilo lilitokea Septemba 27 mwaka huu.
“Hadi sasa Jeshi la Polisi halijui sababu ya kuteketea kwa
gari hilo namba za gari hili hazifahamiki na hata mmiliki wa gari hajajitokeza
Polisi kutoa maelezo ili tuweze kufanya upelelezi wa tukio hili’’, alisema
Kamanda Mushy.
Mushi alisisitiza kuwa maelezo ya mmiliki wa gari hilo kwa
Jeshi la Polisi yatasaidia mchakato wa bima ya gari lililoteketea, kwa sababu bima
haiwezi kutolewa bila kupitia Polisi ambao wanatakiwa kufanya uchunguzi wa
tukio hilo.
Kamanda Mushy ameagiza mabaki ya gari hilo yaliopo katika
eneo la Peramiho jirani na Seminari kuu ya Peramiho yaondolewe kwa kuwa
hayastahili kuendelea kuwepo katika eneo hilo.
Pia amemtaka mmiliki wa gari hilo kujitokeza ili kusaidia
upelelezi na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment