Na Albano Midelo,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imesaini
mkataba wa ukusanyaji ushuru wa mazao wa shilingi milioni 610 na kampuni ya
WOFMAIZE iliyopo hapa Songea.
Makubaliano ya kusaini mkataba huo yamekamilika Oktoba 24
mwaka huu katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Hassan
Mshaweji huku yakishuhudiwa na wawakilishi wa kampuni hiyo pamoja na Kaimu
Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Injinia Samwel Sanya.
Katika mikataba hiyo kampuni hiyo itahusika na ukusanyaji ushuru
wa mazao ya vyakula vilivyosindikwa na visivyosindikwa katika maeneo ya SODECO,
Manzese na maeneo mengine ya Manispaa hiyo.
Mkataba huo ni wa miezi tisa ambao unaanza mwezi Oktoba mwaka
huu hadi Juni 30 mwaka 2018 ambapo kampuni ya WOFMAIZE italipwa asilimia ya
makusanyo yote katika kipindi hicho ambayo ni sawa na zaidi ya milioni 90.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Mstahiki Meya
wa Manispaa ya Songea, Mshaweji ameipongeza kampuni hiyo kwa kushinda zabuni ya
ukusanyaji ushuru huo ambapo ameitaka kuzingatia masharti yaliyopo katika
mkataba na kukusanya ushuru kwa uaminifu.
Mkurugenzi wa WOFMAIZE, Wofram Mlowe ameahidi kampuni yake
kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa ili kufikia malengo ya kukusanya milioni 610
au zaidi katika kipindi cha miezi tisa.
Kadhalika Manispaa hiyo imeamua kusaini makubaliano hayo kwa
ajili ya ubinafsishaji wa vyanzo vya mapato katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na
lengo likiwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100.
No comments:
Post a Comment