Ofisi za Halmashauri Manispaa ya Songea. |
Na Albano Midelo,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani hapa, imewaandikia
barua wamiliki wote wa vituo vya kutolea elimu yoyote bila kusajiliwa kuacha
mara moja tabia hiyo, kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi na endapo kutakuwa
na mtu anafanya hivyo atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Idara ya elimu katika Manispaa hiyo imetoa agizo hilo juzi kwa Waratibu
elimu kata wote waliopo kwenye Manispaa ya Songea kusimamia ipasavyo utekelezaji wake ambapo kuanzia mwezi
uliopita Septemba mwaka huu imepigwa marufuku hairuhusiwi mmiliki wa shule au
kituo chochote kile cha kutolea mafunzo ya tuition kutoa masomo bila kusajiliwa.
Imebainisha kuwa kumeibuka taasisi zisizokuwa rasmi na watu
binafsi kuanzisha vituo vya elimu na kujitangaza kwa njia mbalimbali kwamba
wanatoa masomo ya ngazi mbalimbali ya elimu kuanzia elimu ya chekechea, msingi,
sekondari na vyuo.
Kitendo cha kuanzisha vituo hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni
na taratibu husika kwa sababu kuanzisha shule au kituo kuna taratibu zake
ikiwemo kupata usajili wa kisheria na kufuata taratibu nyingine zinazotolewa
mara tu baada ya kupata usajili huo.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia hutoa
taratibu na miongozo ya kufungua na kuendesha shule, vyuo na vituo vya elimu
vya umma na watu binafsi kwa ajili ya kutoa elimu rasmi na isiyokuwa rasmi kwa
wananchi.
Kwa watu ambao wanataka ufafanuzi zaidi wanapaswa kuwasiliana
na Idara ya elimu Manispaa ya Songea au kupitia kitengo chake cha Elimu ya watu
wazima ambao ndiyo wanatoa utaratibu wa jambo hili.
No comments:
Post a Comment