Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa kijiji cha Lukalasi kitongoji cha Ngembambili
kijiji cha Mkako wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamempongeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli kwa kazi anayoendelea
kuifanya ya kuwaibua mafisadi na kuwachukulia hatua wakiwemo wezi wa madini.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na wachimbaji wadogo wa
madini ambao wanaishi katika maeneo hayo mbele ya mkutano wa hadhara ambao
ulihudhuriwa na Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge.
Masha Mussa na Silvano Challe wakazi wa Ngembambili kwa nyakati
tofauti walisema kuwa kitendo anachokifanya Magufuli na kuwabana mafisadi hao
ambao walikuwa wanadhoofisha uchumi wa nchi, ni ujasiri wa hali ya juu hivyo
wamemwomba aendelee kukaza kamba zaidi ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo viovu
visiweze kuendelea kutokea.
Aidha Challe alimwomba Mkuu huyo wa mkoa kuwabana wachimbaji
wadogo wa madini wa eneo hilo la Ngembambili ambao wanakwepa kulipa kodi ya Serikali
na ikiwezekana wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo jambo ambalo lilimlazimu
mmiliki wa eneo la kuchimba madini aina ya Vito, Sighe Mahundi kukiri mbele ya Dokta
Mahenge kuwa kwa muda wa miaka miwili sasa alikuwa hajalipia leseni ya kuchimba
madini katika eneo hilo.
Pia alisema kuwa wanaiomba Serikali kuona umuhimu wa
kuwaletea umeme kwenye kijiji hicho, ambao utaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa
katika ufanyaji wa kazi zao kwani kijiji hicho kuna mgodi wa uchimbaji wa dhahabu,
taasisi mbalimbali pamoja na wananchi ambao wanahitaji huduma hiyo ya umeme.
“tunaipongeza Serikali kwa kuweka pia miundombinu mizuri ya
barabara ya kutoka Mkako hadi hapa Lukalasi hivyo tunaomba mradi wa Umeme Vijijini
(REA) kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi wa Lukalasi”, alisema.
Mmiliki wa mgodi wa dhahabu uliopo lukalasi Johnson Nchimbi
alimweleza Mkuu wa mkoa, Dokta Mahenge kuwa kwa muda mrefu mgodi wake umekuwa
ukifanya kazi chini ya kiwango kwa sababu kunatatizo kubwa la umeme kwani
wamekuwa wakitumia umeme wa jenereta hivyo endapo umeme wa REA utawafikia wataweza
kuongeza uzalishaji mkubwa wa madini hayo na ameiomba Serikali kutekeleza hilo
ili waweze kuondokana na adha kubwa wanayoipata hivi sasa.
Kwa upande wake Dokta Mahenge alitoa muda wa siku mbili kwa
wachimbaji hao wa madini ambao walikuwa hawalipi leseni walipe kwa kufuata taratibu
zilizowekwa na Serikali huku akimwagiza Kamishna msaidizi wa madini Kanda ya
ziwa Nyasa, Mhandisi Mahobe kuhakikisha kwamba ofisi yake inasimamia kikamilifu
suala hilo ili Serikali iweze kupata mapato yake.
Alisema kuwa mkoa wa Ruvuma unahazina kubwa ya madini ya
dhahabu, shaba, chuma, vito, madini ya viwandani, mawe, kokoto, nishati na urenium
huku akiwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mkoa huo kuona umuhimu wa
kusimamia kikamilifu rasilimali hizo zilizopo kwenye maeneo yao kwa lengo la kudhibiti
pia wanaokwepa kulipia leseni zao za uchimbaji.
No comments:
Post a Comment