Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea, Mameritha Basike akionesha kwa waandishi wa habari mafuta feki ya Albino ambayo yalikamatwa katika moja ya duka linalouza vipodozi mjini hapa. |
Baadhi ya vyakula vilivyoharibika na mafuta feki ya albino ambavyo vilikamatwa hivi karibuni na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Songea. |
Na Albano Midelo,
Songea.
IDARA ya Afya katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa
kushirikiana na watalaamu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wamefanya Operesheni katika maduka ya vipodozi katika mji wa Songea mkoani humo na
kufanikiwa kukamata mafuta ya Albino yakiuzwa kinyume cha sheria na taratibu
husika.
Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dokta Mameritha Basike alisema
mafuta hayo yalikamatwa juzi katika duka la Godluck Mranga ambayo yalikuwa yanauzwa
shilingi 4,500.
“Hairuhusiwi mafuta ya kupaka Albino aina ya Sunblock Cream
UV40 kuwepo kwenye maduka ya vipodozi badala yake mafuta haya yanaruhusiwa
kuwepo kwenye maduka ya dawa (Pharmacy)”, alisema Dokta Basike.
Alisema katika duka hilo pia vimekamatwa vyakula mbalimbali
vilivyoharibika yakiwemo maziwa ya kopo 12 yenye thamani ya zaidi ya shilingi
200,000 na nyama ya kopo 20 zenye thamani ya shilingi 100,000.
Ofisa Afya wa Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela alisema
mfanyabiashara huyo ametozwa faini ya shilingi 500,000 kulingana na sheria za
TFDA na kwamba ametoa rai kwa wafanyabiashara wengine kuacha kuwauzia wananchi
bidhaa ambazo zimeharibika au kumalizika muda wake.
“Natoa wito kwa wananchi kabla ya kununua bidhaa yoyote
wajiridhishe kwa kusoma tarehe ya kutengenezwa bidhaa na mwisho wa matumizi,
ili kuepuka kununua bidhaa ambazo zimeharibika na kupita muda wake wa matumizi
ambazo zinaweza kuleta athari kiafya kwa mtumiaji”, alisisitiza Mkomela.
Naye mfamasia wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Ndavitu
Sanga alitahadharisha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) katika Manispaa hiyo
kuwepo kwa mafuta feki ya kupaka aina ya Sunblock Cream UV40 kwa ajili ya
Albino yanayosaidia kujilinda dhidi ya Saratani ya ngozi.
Kulingana na Sanga alisema kuwa mafuta hayo feki ya Albino yamekuwa
yakiuzwa kati ya shilingi 3,500 hadi 6,000 na kwamba mafuta halisi yamekuwa
yakiuzwa kati ya shilingi 40,000 hadi 90,000.
No comments:
Post a Comment