Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Sheikh
Ponda Issa Ponda amemkosoa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Robert Boaz akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa kuchunguza
matukio ya uhalifu yanayotokea nchini.
Akiwa nchini China kuhudhuria mkutano mkuu wa 86 wa Taasisi
ya Polisi ya Kimataifa (Interpol), Boaz alikaririwa na gazeti moja la Serikali
akisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina uwezo wa kuchunguza matukio ya
uhalifu, yakiwamo mauaji na utekaji bila kusaidiwa na vyombo vya nje.
Hata hivyo, Sheikh Ponda aliyempigia simu jana mwandishi
wetu, alisema kauli iliyotolewa na DCI haina ukweli.
“Kuna matukio mengi ya mauaji na maiti zimekuwa zikiokotwa,
kuna utekaji hadi sasa wengine hawajulikani walipo,” alisema Sheikh Ponda na
kuongeza
“Tunashangaa kumsikia DCI akizungumzia uhodari wa Jeshi la
Polisi katika kuchunguza matukio ya uhalifu, wakati tuna maswali mengi
tunajiuliza.”
Alisema hadi sasa wananchi hawafahamu alipo Ben Saanane,
ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema aliyetoweka tangu Novemba
mwaka jana.
Sheikh Ponda alisema China ni nchi yenye maendeleo katika
masuala ya ulinzi na usalama, hivyo ni vizuri wawakilishi wa Tanzania kwenye
mkutano huo wakaeleza changamoto za usalama zinazotokea nchini ili wasaidiwe
kuongeza ujuzi wa kukabiliana na uhalifu.
Kauli ya Sheikh Ponda imekuja wakati viongozi wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) wakiitaka Serikali iruhusu vyombo vya nje kuchunguza
tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kauli ya Mwigulu;
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema
matukio mengi ya uhalifu yanaendelea kuchunguzwa na akataka jamii kutoa taarifa
ambazo zitasaidia kukamatwa kwa wahusika.
Pia, Nchemba alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama
vina uwezo wa kuchunguza matukio yote, hivyo wachunguzi kutoka nje ya nchi
hawahitajiki. (Muungwana Blog)
No comments:
Post a Comment