Friday, October 6, 2017

OFISI YA KATA MJIMWEMA SONGEA YAGHARIMU UJENZI WAKE MILIONI 25.5

Ofisi ya kata Mjimwema Songea.
Na Albano Midelo,
Songea.

MRADI wa ujenzi Ofisi ya Kata Mjimwema iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umegharimu shilingi milioni 25.56 ambapo ujenzi huo umetokana na fedha zilizotolewa na michango ya wananchi na serikali.

Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Stan Kibiki alisema kuwa kati ya fedha hizo nguvu ya wananchi ni shilingi 556,000 na gharama ya serikali ni shilingi milioni 25.

Vilevile alisema mradi wa ujenzi ya ofisi hiyo ulianza tangu mwaka wa fedha wa 2012/2013 ambapo amezitaja shughuli ambazo zilifanyika katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na kusafisha eneo la mradi, kujenga msingi na kunyanyua ujenzi wa jengo husika.


Kibiki amezitaja kazi zingine ambazo zimefanyika kwa mwaka 2016/2017 kuwa ni ujenzi wa ringbeam, kujenga sehemu zilizosalia ikiwemo sakafu za jengo hilo na kufanya kazi ya kuezeka jengo kwa kutumia bati.


Alisema kata ya Mjimwema ina mitaa mitano na jumla ya wakazi 12,469 ambapo kati yao wanaume ni 5,603 na wanawake ni 6,866.

No comments: