Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema akikagua zana za kufundishia katika Manispaa ya Songea. |
Na Albano Midelo,
Songea.
IMEELEZWA kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma, ina Watu Wazima 2,458 ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Afisa elimu ya Watu Wazima, Faraja Yonas alisema hayo juzi
ambapo alifafanua kuwa kati yao wanaume ni 661 na wanawake ni 1,797.
Yonas alibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za usajili mwezi
Januari hadi Machi mwaka huu, Manispaa hiyo ina jumla ya Watu Wazima 119,328
ambapo kati yao wanaume ni 58,049 na wanawake ni 61,279.
Alisema kuwa hivi sasa Manispaa ya Songea imejipanga vizuri
katika harakati za kuhakikisha kwamba watu wazima wote wanajua kusoma, kuhesabu
na kuandika Kwa asilimia 100.
Anaitaja mikakati ambayo Manispaa inachukua kutekeleza lengo hilo
la Elimu ya Watu Wazima kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Watu Wazima kwa
kuwapatia stadi za kazi muhimu kwa ajili ya kuboresha mipango ya maendeleo
katika sekta hiyo.
Mikakati mingine ni kuongeza ujuzi wa uzalishaji mali na
kuyafahamu mazingira yao kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuweza kuyakabili vyema
mazingira yao na kufikia lengo kuu la Elimu ya Watu Wazima.
Akizungumzia kuhusiana na kisomo chenye manufaa na kisomo cha kujiendeleza na uzalishaji mali
katika Manispaa hiyo, Yonas alisema Manispaa ina vituo 108 vya MUKEJA vyenye
washiriki 2,600, wakiwemo wanaume 937 na wanawake 1,663.
MUKEJA ni Mpango wa uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na
Jamii hivyo katika mpango huu washiriki hujifunza mambo yanayohusu uchumi na
maendeleo ya jamii kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusoma, kuandika na kuhesabu.
Katika mfumo huo washiriki wenyewe ndiyo wanaopanga jambo la
kujifunza, muda muafaka wa kujifunza na namna ya kujifunza na kwamba Mukeja ni
mtaala unaozingatia matakwa ya mwanakisomo katika kujifunza.
Afisa elimu huyo aliongeza kuwa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa
Watoto Waliokosa (MEMKWA) alifafanua kuwa mpango huo unalenga kuwapatia elimu
watoto walioikosa elimu ya msingi, ambao wengi wao wanatoka katika mazingira
magumu au familia zenye kipato duni.
Manispaa ya Songea ina vituo tisa vya MEMKWA, vyenye jumla ya
wanafunzi 103 kati yao wavulana 50 na wasichana 53.
Pia kulingana na maelezo ya Afisa Elimu ya Watu Wazima
alisema Manispaa hiyo ina jumla ya wana kisomo 154 ambapo wanahudhuria masomo, ambapo
hivi sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
Serikali ya Cuba zina mpango wa kutoa Elimu ya Watu Wazima kwa kutumia Redio,
Video na Televisheni.
No comments:
Post a Comment