Monday, April 30, 2018

SERIKALI YAOMBWA KUBORESHA SEKTA YA MICHEZO HAPA NCHINI

Kutoka upande wa kulia aliyesimama ni Mkufunzi wa Mafunzo ya maboresho ya sheria mpya za mpira wa Pete, Yovin Mapunda ambaye ni mwalimu wa Shule ya sekondari Hagati Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, akiwapatia ujuzi baadhi ya walimu wenzake wa Shule za msingi na sekondari katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbinga Mkoani humo, juu ya mabadiliko ya sheria mpya za mpira wa Pete ambapo awali Mapunda alipelekwa Zanzibar kwenye mafunzo hayo ili baadaye aweze kutoa elimu hiyo kwa walimu wengine wanaoendesha michezo mashuleni.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

SERIKALI hapa nchini imeombwa kuboresha sekta ya michezo hasa kwa mpira wa Pete, ili kuweza kuongeza na kuimarisha vipaji vya wachezaji wa mpira huo na kulifanya Taifa liweze kusonga mbele katika michezo.

Aidha Serikali kupitia Waziri wake wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt. Harrison Mwakyembe imeombwa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa michezo katika Shule za msingi na sekondari ili kuweza kuleta mabadiliko yenye tija.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Walimu wa Shule za msingi na Sekondari ambao walishiriki wa mafunzo ya siku tatu, ya maboresho ya sheria mpya za mpira wa pete, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Mbinga iliyopo hapa Mkoani Ruvuma.

UHABA VYUMBA VYA MADARASA WACHANGIA KUSHUKA KIWANGO CHA ELIMU SONGEA


Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

IMEELEZWA kuwa changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi na uhaba wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, imechangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu Wilayani humo, kufuatia ziara iliyofanywa na uongozi wa idara ya elimu katika kata 16 za Halmashauri hiyo kwa lengo la kufanya tathimini ya kubaini changamoto zinazoikumba sekta hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, wadau hao walizitaja changamoto nyingine kuwa ni mwamko hafifu wa wazazi katika kufuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao, wazazi kuhamia mashambani na watoto wao, uhaba wa walimu, uzembe wa walimu kuhudhuria vipindi kwa wakati darasani, kufukuzwa kwa watoto mashuleni, vifo na magonjwa.

Sunday, April 29, 2018

WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MADAWA YA KULEVYA

Mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha kulelea watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Mwangaza mjini Songea Mkoani Ruvuma, Anna Mugenya akiwa amebeba mtoto mchanga ambaye ni wa mwezi mmoja tokea azaliwe ambapo hulelewa kituoni hapo mara baada ya mama yake kufariki dunia alipokuwa amejifungua mtoto huyo.
Na Kassian Nyandindi,  
Songea.

WATOTO yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujiepusha na vitendo viovu vya matumizi ya dawa za kulevya ili wasiweze kuharibu afya zao.

Aidha watoto hao wameaswa kujiepusha na wanaume walaghai ambao wanaweza kuwapotezea ndoto za maisha yao ya baadaye, badala yake wanapaswa kusoma kwa bidii na kuwa viongozi wazuri wa kuliongoza taifa hili.

Mgema alisema hayo juzi alipokuwa kwenye hafla fupi ya kuwaaga watoto hao katika kituo cha Mwangaza, ambao wamefikia ukomo wa kuishi kituoni hapo huku akitoa pongezi kwa uongozi wa kituo kwa kuwasomesha hadi kufikia ngazi ya vyuo vikuu.

SONGEA YAFANIKIWA KUPIGA CHAPA NG'OMBE 12,000


Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imefanikiwa kupiga chapa ng’ombe zaidi ya 12,000 sawa na asilimia 69.6 waliostahili kupigwa chapa hadi kufikia Januari 31 mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simon Bulenganija aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa utekelezaji huo umefanywa, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli la kutaka wapigwe chapa ili kuondoa tabia ya wafugaji kuingiza mifugo bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

“Kati ya ng’ombe 23,000 hapa Songea miongoni mwao ni ng’ombe 12,000 sawa na asilimia 69.6 ndio waliopitiwa na zoezi la upigaji chapa nawaomba wafugaji waendelee kujitokeza kwa wingi kutekeleza zoezi hili”, alisema Bulenganija.

WAJASIRIAMALI WADOGO SONGEA WAPIGWA MSASA


Na Mwandishi wetu,      
Songea.

WAJASIRIAMALI wadogo 380 kutoka vikundi 67 vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepata mafunzo juu ya mbinu za uwekezaji katika viwanda vidogo.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu uliopo mjini hapa, yaliratibiwa na idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo na kufundishwa na watalaam mbalimbali wa taasisi na asasi za kifedha.

Akisoma taarifa ya vikundi hivyo Mkuu wa idara hiyo, Naftari Saioloyi alisema kuwa Manispaa ya Songea imekuwa na utaratibu wa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana kutoka katika mapato yake ya ndani.

Tuesday, April 24, 2018

UKOSEFU WA GARI CHANGAMOTO INAYOKWAMISHA UTENDAJI KAZI KITENGO CHA UZAZI NA MTOTO MBINGA

Baadhi ya Wananchi waliokusanyika jana mjini hapa katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, siku ya uzinduzi wa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

UKOSEFU wa gari maalum la kusambazia chanjo na vifaa tiba vya kutolea huduma, imeelezwa kuwa ni changamoto kubwa inayoikabili idara ya afya kitengo cha huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika vituo vya afya, vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.

Kufuatia uwepo wa tatizo hilo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeombwa kumaliza kero hiyo ndani ya Halmashauri hiyo ili kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi kwa idara hiyo katika jamii.

Hayo yalisemwa na Muuguzi wa afya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga, Verena Mapunda alipokuwa akisoma risala ya uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani kwa Halmashauri ya Mji huo uliofanyika mjini hapa.

RC RUVUMA AWATAKA VIONGOZI WAZAZI KUPIGA VITA MIMBA ZA UTOTONI


Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

SERIKALI katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi kufikia Machi mwaka huu, tayari imetumia jumla ya Shilingi bilioni 4,894,932.063 Mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuboresha mazingira ya elimu.
Christine Mndeme.

Aidha huo ni mkakati wake wa kuwezesha mpango wa elimu bila malipo kwa shule za Msingi na Sekondari Mkoani humo uweze kuwa endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme alisema hayo alipokuwa akizungumza na Wadau mbalimbali wa elimu Mkoani hapa katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.

Alisema kuwa ni jambo la kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini ambapo ameweza pia kutoa vifaa vya maabara kwenye shule za Serikali, jambo ambalo sasa linasaidia watoto shuleni waweze kusoma masomo ya Sayansi kwa vitendo bila usumbufu wa aina yoyote ile.

WANACHAMA WA USHIRIKA TUNDURU WAASWA


Na Dustan Ndunguru,    
Tunduru.

VIONGOZI wa vyama vya ushirika Wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kusimamia kikamilifu hesabu za vyama hivyo, ili viweze kuwanufaisha wanachama wake na kuvifanya kuwa endelevu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera alisema kuwa viongozi wengi wa vyama ushirika hapa nchini wamekuwa legelege katika kufuatilia mikopo wanayotoa kwa wanachama wao, na kushindwa kusimamia hesabu ipasavyo za uendeshaji wa ushirika huo na mwisho wa siku husababisha kuyumba na kufa kabisa kwa vyama vya ushirika.

Alisema kuwa wanachama wa vyama hivyo wanatakiwa kujenga mazoea ya kulipa mikopo waliyokopeshwa kwa wakati, ili kuweza kutoa nafasi kwa wanachama wengine waweze kukopa.

Saturday, April 21, 2018

MANISPAA SONGEA WAPATIWA MAFUNZO UTOAJI CHANJO SARATANI MLANGO WA KIZAZI

Walimu wa afya katika shule za Msingi na Sekondari na Wahudumu wa afya kutoka katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wakipata mafunzo ya utoaji wa chanjo ya Saratani mlango wa kizazi katika ukumbi wa Manispaa hiyo, ili waweze kwenda kuwahudumia Watoto wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14.

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MAFUNZO ya utoaji wa Chanjo ya Saratani mlango wa kizazi, kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14 yamefanyika katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Aidha mafunzo hayo yameshirikisha Walimu wa afya kutoka shule za Msingi na Sekondari na Wahudumu wa afya ya msingi zaidi ya 300 kutoka katika Manispaa hiyo mjini hapa.

Kufanyika kwa zoezi hilo kunalenga kwamba kabla ya siku ya Jumatatu Aprili 23 mwaka huu, siku hiyo utafanyika uzinduzi wa Mkoa huo wa chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri huo.

Friday, April 20, 2018

MACHINJIO HALMASHAURI MJI WA MBINGA YALALAMIKIWA KUKOSA MAJI YAKITHIRI KWA UCHAFU

Machinjio ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, ambayo inalalamikiwa kukosa huduma ya maji na kushamiri kwa uchafu.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WACHINJAJI wa ng’ombe katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wamesema kwamba wanashindwa kufanya kazi ya uchinjaji ng’ombe katika machinjio ya Halmashauri hiyo, iliyopo mjini hapa kutokana na kukosa huduma ya maji.

Aidha kufuatia uwepo wa tatizo la ukosefu wa huduma hiyo muhimu machinjio hiyo imekuwa katika hali mbaya kutokana na kukithiri kwa uchafu.

Wauzaji wa nyama ya ng’ombe mjini hapa nao jana wametia mgomo wa muda usiojulikana wakikataa kutoa huduma ya uchinjaji na uuzaji nyama, mpaka Mamlaka husika itakapoweza kutatua tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu na kuwa kero kubwa.

MAKALA: KALINGA MILLERS MFANO WA KUIGWA MKOANI RUVUMA

Baadhi ya Wafanyakazi wa kiwanda kidogo cha Kalinga Millers, ambacho husindika unga wa Mahindi kilichopo Songea mjini Mkoani Ruvuma.
Unga wa Mahindi uliosindikwa na Kalinga Millers.

Na Dustan Ndunguru,

SERIKALI ya awamu ya tano imedhamiria Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, juhudi zinazoendelea hivi sasa ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda hivyo kuanzia vidogo hadi vikubwa, hali ambayo itasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira katika jamii.

Katika kuhakikisha mchakato huo unakuwa wenye ufanisi kunahitajika mipango mahusus ya kujenga viwanda vidogo, ukizingatia kwamba hasa katika sekta ya kilimo ndiko ambako malighafi huzalishwa kwa wingi.

Tunatambua ili viwanda hivyo viweze kuanzishwa kwa wingi hususan katika maeneo ya vijijini, miundombinu nishati ya umeme inatakiwa ijengwe huko kwa wingi na kwamba wataalamu wa sekta ya kilimo nao wanapaswa kuongeza juhudi katika kuelimisha na kujenga hamasa kwa wakulima waweze kuzalisha mazao ya aina mbalimbali, yenye ubora na hivyo mwisho wa siku kuweza kufanya viwanda vyetu vidogo na vile vikubwa tutakavyoanzisha kuwa endelevu na kuleta manufaa makubwa katika kukuza uchumi wetu.

Wednesday, April 18, 2018

DOKTA MAGUFULI ATOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA MRISHO GAMBO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akiwasili mtaa wa Muheza Kariakoo jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia ya Mzee Mashaka Gambo kwa kufiwa na mkewe ambaye pia ni mama mzazi wa  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kufiwa na mama yake mzazi Marehemu Rehema Paul Mumbuli leo Aprili 18 mwaka huu.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akiweka saini kwenye kitabu cha maombolezo baada ya kuwasili mtaa wa Muheza Kariakoo jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia ya Mzee Mashaka Gambo kwa kufiwa na mkewe ambaye pia ni mama mzazi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akimpa pole Mzee Mashaka Gambo kwa kufiwa na mkewe Marehemu Rehema Paul Mumbuli leo Aprili 18 mwaka huu.

POLEPOLE ATAKA VIONGOZI WANAOPOTOSHA UMMA WACHUKULIWE HATUA


Na Mwandishi wetu,

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey PolePole, amefunguka na kuwavaa viongozi ambao wanazungumza juu ya ripoti ya CAG na kusema baadhi ya viongozi hao wanapotosha umma kwa kusema mambo ya uongo.
Humphrey Polepole.

Polepole alisema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kusema kuwa wapo viongozi wa vyama vya siasa hawazungumzi juu ya mambo mazuri, yaliyofanywa na Serikali kama vile ujenzi wa miundombinu na mambo wanayopiga hatua ila wamekuwa wakidakia mambo na kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli.

“Sasa unaposoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halafu unatoa kauli timilifu kuwa pesa imeibwa, yaani pesa ya umma imeibwa,

Thursday, April 12, 2018

WATU 17 WAPOTEZA MAISHA WENGINE 14 WAJERUHIWA VIBAYA


KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wameripotiwa watu 17 kufariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa vibaya, katika ajali ya basi iliyotokea kwa makosa ya kibinadamu baada ya dereva wa gari hilo kupoteza muelekeo.

Imefafanuliwa kuwa hali hiyo ilitokana na dereva huyo akijaribu kulikwepa Lori lililokuwa likijielekeza katika upande wake.

Mkuu wa Wilaya ya Narok nchini Kenya, George Natembeya alisema kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 63.

DOKTA MAGUFULI AMBADILISHA MPAMBE WAKE WENGINE WAPANDISHWA VYEO


Na Mwandishi wetu,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli, ameridhia kuwapandisha vyeo maofisa 28 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuanzia leo Aprili 12 mwaka huu.

Tukio hilo limeenda sambamba huku akimbadilisha Msaidizi wake Kanali Mbaraka Mkeremy, ambaye amempandisha cheo na atapangiwa kazi nyingine jeshini.

Kadhalika Rais Magufuli amekukubali kumpandisha cheo kutoka Luteni Kanali kuwa kanali D.P.M Murunga na kuwa mpambe wa Rais akichukua nafasi ya Kanali Mkeremy.

Sunday, April 8, 2018

BUSTANI MANISPAA SONGEA KUANZA KUTUMIKA MWEZI UJAO


Mandhari ya bustani ya Manispaa Songea Mkoani Ruvuma.

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MRADI wa bustani ya Manispaa ya Songea uliopo Mkoani Ruvuma, umekamilika na kwamba unatarajia kuanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo Mkandarasi husika tayari amekabidhi mradi huo kwa uongozi wa Manispaa hiyo.

Kaimu Mkuu wa idara ya ujenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi Nicolous Danda alisema kuwa mradi huo ulikamilika tangu mwezi Desemba mwaka 2017 huku Mkandarasi aliyepewa jukumu la ujenzi wa bustani hiyo akipewa matazamio ya miezi sita ya ujenzi wa mradi huo ambayo inaishia mwezi Aprili mwaka huu.

Danda amezitaja kazi zilizosalia katika mradi huo kuwa ni kuendelea kuotesha nyasi, kufunga mfumo wa maji taka ambayo inafanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (SOUWASA) na kuweka nishati ya Umeme kazi ambazo zinatarajia kukamilika mapema mwezi huu.

WACHINA WAANZA UJENZI STENDI MPYA MANISPAA SONGEA


Wataalamu wa Kampuni ya kichini ya SIETCO wakiwa pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Songea, katika eneo la ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi ya abiria ambayo ujenzi wake tayari umekwisha anza. 

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

HATIMAYE Kampuni ya Serikali kutoka nchi ya China inayofahamika kwa jina la, China Sichuan International Cooperation (SIETCO) imewasili mjini Songea tayari kwa kuanza kazi ya ujenzi wa Stendi mpya ya kisasa kwa ajili ya magari ya abiria, katika eneo la Kata ya Tanga Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

SIETCO imesaini mkataba wa miezi 18 kwa ajili ya kazi ya ujenzi huo na Halmashauri ya Manispaa hiyo, kujenga Stendi mpya ya mabasi katika eneo hilo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo ameiambia Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Songea kuwa, wanatarajia kutoa ajira kwa wakazi wa Songea ambapo hivi sasa tayari wametoa ajira kwa wafanyakazi wachache katika hatua za awali kwa ajili ya kuweza kuanza kazi za mradi huo.

Saturday, April 7, 2018

TASAF YAWEZESHA TUWEMACHO TUNDURU UJENZI BWAWA LA MAJI


Na Muhidin Amri,      
Tunduru.

WANANCHI wa Kijiji cha Tuwemacho kata ya Tuwemacho Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hapa nchini, wamefanikiwa kujenga bwawa kubwa la maji safi ili kuweza kumaliza kero ya muda mrefu  ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Kuchimbwa kwa bwawa hilo, kumekuja baada ya vyanzo vya maji vilivyopo kwenye kijiji hicho kushindwa kukidhi mahitaji halisi ya wananchi husika, kutokana na ongezeko kubwa la wageni wanaofika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha zao maarufu la korosho.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Tuwemacho, Ali Fadhil alisema kuwa TASAF kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji hicho, umewezesha kupatikana kwa majawabu mengi ya kero za wananchi ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji.

Friday, April 6, 2018

TUKIO KATIKA PICHA: TASAF YAWAINUA CHINGUNGULU TUNDURU UANZISHAJI MABWAWA YA SAMAKI

Afisa uvuvi wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Rhoda Komanya aliyenyoosha mkono akiwa na Wajumbe wa Serikali ya kijiji cha Chingungulu Wilayani hapa wakiangalia bwala la mradi wa Samaki ambalo linakusudia kuwanufaisha zaidi ya walengwa 111 waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Wilayani humo.

TUWASA TUNDURU YAONGEZA MTANDAO HUDUMA MAJI SAFI NA SALAMA


Na Mwandishi wetu,     
Tunduru.

IDADI ya Wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Tunduru Mkoani Ruvuma, imeongezeka kutoka 23,200 mwaka 2016/2017 hadi kufikia wananchi 32,200 katika kipindi cha mwaka huu.

Aidha kutokana na maboresho ya mitambo na vyanzo vya maji yanayoendelea kufanywa na Mamlaka  ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Tunduru (TUWASA) hivi sasa mgawo wa maji umepungua kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Jeshi la magereza, Hospitali ya Wilaya, kambi ya Polisi na maeneo mengine katika mji huo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mamlaka hiyo, Christopher Mbunda wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa, ambapo  alisema TUWASA imeweza kuwa na wateja 1,590 na kati ya hao waliofungiwa mita ni 1,460 na wasio na mita ni 130.

WANUFAIKA TASAF TUNDURU WAANZISHA SHAMBA LA MITI YA MBAO


Na Kassian Nyandindi,         
Tunduru.

WALENGWA waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kijiji cha Mchesi kata ya Mchesi, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma kupitia ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameanzisha shamba la miti ya mbao, aina ya Mitiki lenye ukubwa wa ekari nne.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho ambaye pia ni mlezi wa wanufaika hao waliopo katika mpango huo, Lazima Mrope alisema kuwa katika ekari hizo tayari wamepanda jumla ya miti 1,200 ya mbao kati ya miti 4,000 iliyopo kwenye mpango wa kuipanda ikiwemo miti ya matunda na kwamba miti iliyobaki imegawiwa bure kwa wanufaika ambao wamepanda katika mashamba yao binafsi.

Mrope alifafanua kuwa mbali na miti hiyo ya mbao pia wameanzisha kilimo cha mahindi, ambayo mara yatakapokomaa wanufaika watakuwa na uhakika wa kuweza kupata chakula katika msimu wote wa mwaka, badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali ambayo hata hivyo haitoshelezi mahitaji yao.

Wednesday, April 4, 2018

NAMTUMBO YAPOKEA MILIONI 400 UJENZI MAJENGO KITUO CHA AFYA


Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

HALMASHAURI Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, imepokea fedha Shilingi milioni 400 kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya kuongeza, ujenzi wa majengo manne ya Kituo cha afya Namtumbo kilichopo Wilayani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Halmashauri hiyo inaeleza kuwa walipokea fedha hizo, mwezi Novemba mwaka jana na kwamba baada ya kutolewa taratibu za miongozo husika juu ya matumizi hayo utekelezaji unafanyika ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Baada ya kupitia miongozo ya matumizi ya fedha hizo Halmashauri imeanza ujenzi wa majengo hayo, katika Kituo cha afya Namtumbo kilichopo katika kata ya Rwinga mjini hapa.

TFS YAPANDA MITI HEKTA 1,630 MADABA WANANCHI WAPEWA MICHE BURE


Na Muhidin Amri,   
Madaba.

WAKALA wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) kupitia shamba la miti Wino lililopo katika kata ya Wino Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 Wakala huyo ameweza kupanda hekta 1,630 za miti ya aina mbalimbali.

Mbali na kupanda idadi ya miti hiyo, amefanikiwa kutoa miche ya miti bure kwa wananchi na vikundi vilivyoamua kuanzisha mashamba ya miti kibiashara, ili waweze kujikwamua na umaskini baada ya kuonekana kwamba zao la miti lina soko kubwa hapa nchini.

Kaimu Meneja wa shamba hilo, Haji Mpya alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Wino, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.

Monday, April 2, 2018

MIKOA INAYOONGOZA KWA UTORO WA WANAFUNZI HII HAPA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Na Mwandishi wetu,

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaja Mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga kuwa ndiyo inayoongoza kwa utoro wa wanafunzi wa Sekondari hapa nchini.

Majaliwa ameitaja pia Mikoa ya Rukwa, Geita, Tabora, Singida na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi.

Alisema hayo leo Aprili 2 mwaka huu, wakati wa uzinduzi Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kwenye uwanja wa Magogo Mkoani Geita.

Sunday, April 1, 2018

DOKTA MAGUFULI AWATAKIA WATANZANIA HERI YA SIKUKUU YA PASAKA


Na Mwandishi wetu, 


RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli leo Aprili Mosi mwaka huu ameungana na Wakristo wote katika maadhimisho ya Misa Takatifu, ya sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukaribishwa na Padri Venance Tegete kutoa salamu, Dokta Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya sikukuu hiyo huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani, upendo na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa hili.

“Kifo na ufufuko wa bwana wetu Yesu Kristo ukafufue matendo yetu, tuendelee kuijenga amani yetu, upendo wetu na tujenge maendeleo ya Watanzania wote, kwani Kristo alitufundisha upendo miongoni mwetu,

BREAKING NEWS: MZIMU WA UBADHIRIFU FEDHA ZA WANACHAMA WAENDELEA KUITAFUNA MBINGA TEACHERS SACCOS

Baadhi ya Wanachama wa Mbinga Teachers SACCOS, Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma wakiwa jana kwenye Mkutano wao wa uchaguzi, ambao haukufanyika kutokana na idadi kamili ya wanachama wenzao kutotimia.

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

MKUTANO Mkuu wa uchaguzi wa kuwachagua Viongozi wapya wa Chama cha Akiba na Mikopo, Mbinga Teachers SACCOS Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma jana Machi 31 mwaka huu, umeshindwa kufanyika kutokana na idadi kamili ya Wanachama wa Chama hicho kushindwa kuhudhuria katika mkutano huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndani ya ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa ambako Mkutano huo ulitarajiwa kufanyika hapo, baadhi ya Wanachama wa chama hicho walisema kuwa tatizo hilo limesababishwa na wanachama wenzao kukata tamaa ya kuendelea kuwa wanachama ndani ya ushirika huo kutokana na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha, uliofanywa na viongozi husika waliopewa dhamana ya kuendesha umoja wao.

Walisema kuwa licha ya kutoa kilio chao kwa muda mrefu wakitaka vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla, iingilie kati kupitia Mrajisi wa Vyama vya ushirika Mkoani Ruvuma ili kuweza kunusuru mali na fedha zao, hali hiyo bado imekuwa mbaya na ndiyo maana wamekata tamaa.

UHAMASISHAJI ELIMU YA KUJITOLEA DAMU NI LAZIMA



Na Albano Midelo,    
Songea.

MANISPAA ya Songea Mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, wiki ya mwisho wa mwezi Machi mwaka huu iliweka kituo cha wananchi kujitolea damu katika viwanja vya Soko kuu mjini Songea. 

Uchunguzi umebaini kuwa asilimia 80 ya wanaohitaji damu hapa nchini ni wanawake, kwa sababu mbalimbali ikiwemo uzazi salama wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida na njia ya upasuaji. 

Katika kipindi cha siku tatu za uhamasishaji wa wananchi kujitolea damu, lengo lilikuwa ni kukusanya uniti 100 za damu.