Tangaza Biashara yako nasi kwa Matangazo ya aina mbalimbali, Mawasiliano zaidi piga simu namba 0762 578960
Tuesday, February 16, 2016
SERIKALI YAPELEKA TANI 200 ZA MAHINDI KWA AJILI YA CHAKULA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI
Na Mwandishi Maalum,
Rufiji.
SERIKALI imepeleka tani 200
za mahindi ya chakula cha msaada kwa waathirika wa maafa waliokumbwa na
mafuriko wilayani Rufiji mkoa wa Pwani, yaliyotokea huko na kuathiri jamii
ikiwemo uharibifu wa mashamba na chakula cha akiba cha wananchi waishio tarafa
ya Mkongo, Ikwiriri na Mhoro wilaya humo.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara ya
kukagua athari za maafa hayo Februari 16 mwaka huu, Waziri wa nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu sera, bunge, ajira na wenye ulemavu, Jenista Mhagama alibainisha
kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha kwamba inawajengea uwezo wananchi wake,
pindi maafa yanapotokea.
“Ndugu zangu wanarufiji awali maafa yalipotokea hapa wilayani,
tulitanguliza tani 100 za mahindi na sasa tunaongeza nyingine 200 hivyo
tutakuwa tumeleta jumla ya tani 300 lakini hatutaishia hapo, tumewaleta sasa na
mbegu za mahindi tani 3 na mtama tani 2 lengo la serikali tumieni mbegu hizi
kuzalisha mazao kwani yenyewe haiwezi kuwalisha katika kipindi cha mwaka mzima,
mkitumia mahindi haya mtaweza kukabiliana na upungufu wa chakula unaowakabili”,
alisema Mhagama.
| Mkazi wa kijiji cha Mayuyu wilayani Rufiji, Suleiman Idd akiishukuru serikali kwa msaada huo. |
Waziri Mhagama aliongeza kuwa pamoja na serikali kupeleka
mahindi hayo katika wilaya ya Rufiji, bado wataalamu wake wanaendelea na
tathimini ya kina ili kuweza kufanya upembuzi yakinifu juu ya mahitaji halisi ya
chakula na mbegu wilayani humo, lengo ikiwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wa
wilaya hiyo wanakuwa na chakula cha kutosha.
Monday, February 15, 2016
SERIKALI KUPELEKA MADAKTARI BINGWA MAENEO YA PEMBEZONI IKIWEMO MKOA WA RUVUMA
Na Mwandishi wetu,
Songea.
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt.
Hamis Kigwangalla amesema wizara yake itahakikisha inapeleka Madaktari bingwa
katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ikiwemo hospitali ya mkoa wa Ruvuma, ili
kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi katika sekta hiyo ya afya.
Hayo yalisemwa na Dkt. Kigwangalla wakati alipokuwa katika
ziara yake mkoani humo, aliyoifanya mapema hivi karibuni Februari 13 mwaka huu.
WATUMISHI WANNE HALMASHAURI SONGEA WATUMBULIWA MAJIPU
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATUMISHI wanne waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kazi na Baraza la Madiwani wa Halmashauri
hiyo kutokana na utovu wa nidhamu, wakidaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha na
kushindwa kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi za utumishi wa umma.
Imefafanuliwa kuwa waliosimamishwa kazi kuwa ni wa idara ya
ujenzi, maji, ushirika pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Songea, Rajabu Mtiula alisema kuwa baraza lake limefikia
maamuzi hayo baada ya kuridhika na taarifa ya kamati ya fedha, uchumi na
mipango kwamba watumishi hao, wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao na
kuisababishia hasara halmashauri hiyo.
Mtiula aliwataja watumishi waliosimamishwa kuwa ni mhandisi
wa ujenzi Daud Basilio, mhandisi wa maji John Undili, ofisa ushirika
Sheken Masawe pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Hotay Thuway ambapo
kila mmoja alikuwa na tuhuma zake za ubadhirifu.
SERIKALI MKOANI IRINGA YAAGIZA KUFUNGWA KWA SHULE ZA MSINGI KUTOKANA NA MLIPUKO WA KIPINDUPINDU
Iringa.
SERIKALI mkoani Iringa imeagiza kufungwa
kwa shule zote za msingi, katika kata tatu za tarafa ya Pawaga
baada ya moja ya vijiji vyake, kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa kipindupindu.
Mpaka jana idadi ya watu waliopatwa na maambukizi ya ugonjwa
huo, iliongezeka hadi 161 kutoka watu 85 walioripotiwa juzi huku mapambano
dhidi ya ugonjwa huo, yakiendelea pamoja na baadhi ya wananchi wa vitongoji vya
tarafa hiyo kuzingirwa na maji kutokana na mafuriko.
| Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza. |
Mbali na kuagiza shule hizo zifungwe, Mkuu wa Mkoa wa Iringa
Amina Masenza amewataka wenye mashamba ya mpunga katika kijiji cha
Mboliboli ambacho ugonjwa huo umelipuka, kujitokeza mara moja ili
kuisadia serikali kuwaondoa vibarua waliobaki katika mashamba yao ili
wasalimike na maambukizi yake.
Alisema vibarua katika mashamba hayo wanatoka katika
wilaya za Kilolo mkoani Iringa, huku wengine wakiripoti kutoka katika mikoa ya
Mbeya na Morogoro.
MKURUGENZI WA KANDA MSD NA WENZAKE WASIMAMISHWA KAZI
![]() |
| Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. |
Dar es Salaam,
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Kanda, huduma kwa wateja Bohari kuu ya Dawa (MSD) hapa nchini, Cosmas
Mwaifwani (pichani juu) na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi bilioni
1.5.
Sunday, February 14, 2016
TASAF MBINGA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE WANUFAIKA WAISHUKURU SERIKALI
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANUFAIKA waliopo kwenye mpango wa uhaulishaji fedha, kaya
maskini katika wilaya ya Mbinga vijijini na Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu
ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa kubuni na kuwapelekea mradi
huo katika maeneo yao mbalimbali wilayani humo.
Jumla ya kaya 10,436 zilizopo katika kata zote za wilaya
hizo, zimewezeshwa fedha shilingi milioni 394,972,000 kwa ajili ya huduma za
afya, elimu na kupewa ruzuku ya msingi ambayo huwawezesha kujiongezea kipato
katika maisha yao ya kila siku.
![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini, Ladislaus Mwamanga. |
Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo
wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea
fedha hizo kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, nguruwe, samaki, kuku, na matibabu
huku wengine wakinunua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.
Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye
mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea vijiji vya Lazi, Mpapa,
Ruanda, Mkwaya na Chunya wilayani humo.
Wakifafanua maelezo yao kwa nyakati tofauti, wanufaika hao
walisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo hadi sasa baadhi yao wameweza kumudu
gharama za maisha yao ikiwemo kujikwamua na umaskini waliokuwa nao, hususani
katika suala zima la kupeleka watoto wao shule.
WASIOPELEKA WATOTO WAO SHULE SONGEA WATAFUTIWA MWAROBAINI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya
amewataka wazazi ambao hawajapeleka watoto wao shule wilayani humo watekeleze
agizo la serikali la kupeleka watoto hao shule haraka iwezekanavyo, ifikapo
mwishoni mwa mwezi huu kabla hawaja chukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo
kufikishwa Mahakamani.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu huyo wa wilaya, alipokuwa kwenye
ziara yake ya kikazi katika kata ya Mpitimbi na Litapwasi wilayani humo akizungumza
na wazazi, walimu, watendaji wa vijiji na kata pamoja na madiwani.
Aidha aliwataka watendaji wa kata na vijiji wakiwemo maofisa
tarafa wilayani Songea kwamba, ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wahakikishe
watoto wote waliochaguliwa kuanza elimu ya msingi na sekondari ambao hawaja
ripoti shule, wakamatwe mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Saturday, February 13, 2016
JIPU LATUMBULIWA SONGEA MHANDISI WA UJENZI ASIMAMISHWA KAZI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kupitia baraza
lake la Madiwani wa Halmashauri hiyo limemsimamisha kazi Mhandisi wa idara ya
ujenzi Daud Basilio, kwa sababu ya uzembe wa kutokuwa kazini kwa muda mrefu,
ubadhirifu wa fedha na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya idara
hiyo.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari ofisini
kwake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Rajabu Mtiula alisema, pia wamechukua
hatua hiyo baada ya mhandisi huyo, kuisababishia halmashauri hasara ya shilingi
milioni 38,186,400.
![]() |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Mtiula alisema kuwa katika kikao chake cha dharula
kilichoketi juzi mjini hapa, kimeamua kumweka pembeni mhandisi Basilio kutokana
na licha ya kuonywa mara kwa mara na baraza hilo la madiwani, amekuwa akipuuza
na kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, ikiwemo kushindwa kusimamia
kikamilifu miradi mbalimbali ya wananchi inayotekelezwa katika idara ya ujenzi.
Alifafanua kuwa mhandisi huyo, amekuwa akitumia taaluma yake
vibaya ambapo amekuwa akishirikiana na wakandarasi kuihujumu halmashauri na
kuisababishia hasara kubwa ya fedha, kitendo ambacho kinawakosesha wananchi kupata
huduma stahiki.
MIEZI SITA JELA KWA KUMILIKI SILAHA KINYUME NA TARATIBU ZA NCHI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja anayeishi mtaa wa Misufini Tunduru mjini hapa mkoani
Ruvuma, Mohamed Rashid Linyama (42) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita
jela baada ya kupatikana kosa la kukutwa na silaha kinyume cha
sheria na taratibu za nchi, juu ya umiliki halali wa silaha na risasi zake.
Adhabu hiyo imetolewa na Mahakama ya wilaya ya Tunduru, na
kutoa amri ya kutaifishwa kwa bunduki hiyo na kuwa mali ya serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy alitoa
hukumu hiyo baada ya mtuhumiwa kukiri kufanya kosa hilo na kuifanya Mahakama kumtia
hatiani kwa kosa lililokuwa likimkabili.
Awali akisoma shikata hilo lenye jinai namba 4/2016 mwendesha
mashtaka wa Mahakama hiyo, mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelael
Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Disemba 31 mwaka jana, akiwa
na bunduki katika kijiji cha Likweso majira ya asubuhi.
Katika hati ya mashtaka hayo mtuhumiwa Linyama pia alikuwa
na shitaka namba 2/2016 lililokuwa likimkabili juu ya wizi wa pikipiki aina ya
Sunlg, yenye namba za usajili MC 670 ACG aliyokutwa akiwa anaitumia siku
alipokamatwa na bunduki hiyo, kosa ambalo nalo liliondolewa baada ya mmliki wa
pikipiki hiyo, kujitokeza na kukabidhiwa.
WATENDAJI WAPANDISHWA KIZIMBANI TUNDURU KWA WIZI WA PEMBEJEO ZA KILIMO
Na Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewafikisha
Mahakamani watendaji wake sita wa wilaya hiyo, wakituhumiwa kuhujumu mfumo wa
ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima.
Watendaji hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
wilaya hiyo, na kwamba kila mmoja wao, anatuhuma ya kujibu makosa mawili
yanayowakabili Mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka yao, watuhumiwa hao
wanakabiliwa na makosa ya kula njama kinyume na kifungu cha sheria namba 384
cha sheria za kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Vilevile kwa kosa la pili linalowakabili ni kwamba, watendaji
hao wametumia mbinu za wizi kuiba vocha za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zilizopangwa kuwapelekea wanufaika yaani wakulima, kupitia mfumo wa ruzuku
wa pembejeo za kilimo.
Friday, February 12, 2016
SERIKALI YAWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI WAKALA WA VIPIMO HAPA NCHINI
Dar es Salaam,
SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka
Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo hii, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa
mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka
mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo
nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi.
Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta
bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu
kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini
Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi
ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote
hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi
ziendelee,” alisema.
MKUU WA WILAYA MBINGA AWATAKA VIONGOZI KUACHA TABIA YA KUJIKWEZA NA KUWA MIUNGU WATU
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SENYI Ngaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuacha tabia ya kujikweza na kuwa miungu watu
badala yake wajenge ushirikiano na wananchi katika kutatua kero mbalimbali kwa
wakati, ili waweze kuendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali hii ya awamu
ya tano.
Ngaga alisema kuwa ni jukumu la kila kiongozi wilayani humo kujituma
kikamilifu katika utekelezaji majukumu ya wananchi, huku akisisitiza suala la
ukusanyaji wa mapato kikamilifu na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato hayo.
| Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga. |
“Mkurugenzi na wataalamu wako, nawaagiza simamieni kikamilifu
kipengele hiki cha ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa ambayo
serikali imeagiza, pia kuweni wabunifu
wa vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kuongeza kiasi cha fedha ambazo zitaweza
kuhudumia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo”, alisisitiza Ngaga.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alitoa rai hiyo juzi alipokuwa
akitoa salamu za serikali katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la wilaya
hiyo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Thursday, February 11, 2016
WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA BANDARINI AMPA MASAA MANNE MTENDAJI MKUU WAKALA WA VIPIMO AANDIKE BARUA YA KUJIELEZA
Dar es Salaam,
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara ya
ghafla kwenye kitengo cha upimaji mafuta bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta
zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea
mita za kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa Kigamboni.
Aidha, Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya
kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka
mitano iliyopita na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
“Nataka unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya
kufunga mita hizo, na kwa nini jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini
umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms)
wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua
kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi
rasmi?” alisema Waziri Mkuu.
“Umesema mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa
kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au
kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka
kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye
mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na
siyo mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.
MADIWANI SONGEA WATUMBUA JIPU WAMSIMAMISHA KAZI MHANDISI MAJI KUTOKANA NA UZEMBE KAZINI
![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
BARAZA la Madiwani Halmashauri wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,
limemsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo, John Undili
kwa sababu ya uzembe na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya
maji na kuisababishia Halmashauri hiyo, hasara ya mamilioni ya fedha.
Akitoa taarifa hiyo kwenye baraza hilo lililoketi mjini hapa,
Mwenyekiti wake Rajabu Mtiula alisema mhandisi huyo licha ya kuonywa mara kwa
mara na baraza lake, amekuwa akipuuza kutekeleza wajibu wake wa utumishi wa
umma na maelekezo anayopewa na viongozi wake wa ngazi ya juu ndani ya
halmashauri hiyo.
Mwenyekiti huyo alifafanua kwamba waliona ni vyema achukuliwe
hatua hiyo ya kinidhamu, ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea na iwe
fundisho kwa watumishi wengine wa wilaya hiyo, wenye tabia ya kuzembea kutimiza
majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Mtiula ambaye pia ni Diwani wa kata ya Litapwasi, alibainisha
kuwa Mhandisi huyo alishindwa kusimamia miradi ya maji katika kipindi cha
kuanzia Januari hadi Disemba mwaka jana, kitendo ambacho kimesababisha hata wananchi
wake wakose huduma ya maji safi na salama.
MAHABUSU ALIYEJINYONGA NAMTUMBO UTATA MTUPU
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MTUHUMIWA mmoja ambaye aliwekwa rumande katika mahabusu ya
kituo kidogo cha Polisi kata ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, amekutwa
akiwa amejinyonga na kufariki dunia, ndani ya chumba cha mahabusu hiyo.
Taarifa za tukio hilo zinafafanua kuwa, Vumi Issa Kasumali (30)
ambaye ni mkazi wa kata ya Msisima wilayani humo, ndiye aliyepoteza uhai wake kwa
kujinyonga kwa kutumia suruali, aliyokuwa amevaa mwilini mwake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji
amethibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kwamba, lilitokea majira ya mchana
Februari 9 mwaka huu.
Mwombeji alieleza kuwa mtuhumiwa huyo, alikuwa anakabiliwa na
tuhuma ya kuvunja nyumba na kuiba na kwamba wakati anachukua maamuzi magumu ya
kujiua, askari Polisi walikuwa wanajiandaa kumsafirisha kwenda Mahakama ya
wilaya Namtumbo ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
MADIWANI MBINGA WAPITISHA BAJETI SHILINGI BILIONI 49.4 KWA AJILI YA UTEKELEZAJI MAENDELEO YA WANANCHI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika rasimu
yake ya bajeti ya mwaka 2016/2017 imekisia kukusanya na kutumia kiasi cha
shilingi bilioni 49.4 kwa ajili ya utekelezaji na kuboresha shughuli mbalimbali,
za maendeleo ya wananchi wilayani humo.
Katika fedha hizo shilingi bilioni 32.5 zinalenga kulipa
mishahara ya wafanyakazi wake, bilioni 3.9 matumizi mengine, bilioni 9.0 ni
fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha imekisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 3.8
ambazo ni fedha zitakazotokana na makusanyo ya ndani, katika halmashauri ya
wilaya hiyo.
Tuesday, February 9, 2016
WANAFUNZI NAKAPANYA TUNDURU WAISHI KWA HOFU KUTOKANA NA KUSUMBULIWA NA HOMA YA MATUMBO
| Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu. |
Na Steven Chindiye,
Tunduru.
WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya Sekondari Nakapanya
Wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanaishi kwa hofu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa
wa homa ya matumbo ambayo imezuka shuleni hapo.
Hayo yalibainishwa na wananafunzi hao, walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wa habari hizi na kuongeza kuwa, hofu hiyo imetokana
na wenzao 56 kuanza kuugua ugonjwa wa kuharisha mfululizo.
Walisema kufuatia mlipuko huo, timu ya wataalamu wa afya kutoka
hospitali ya wilaya hiyo ikiongozwa na Kaimu mganga mkuu wa wilaya, Dkt. Bernad
Mwamanda walienda huko na kutoa huduma kwa wagonjwa walioathirika ambapo pamoja
na mambo mengine, timu hiyo pia ilichukua sampuli kwa ajili ya kwenda kufanyia
uchunguzi zaidi ili kuweza kutafuta na kupatikana ufumbuzi wa tatizo hilo.
MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKALI YABOMOA NYUMBA ZA WANANCHI TUNDURU WAKOSA MAHALI PA KUISHI
Na Steven Chindiye,
Tunduru.
MVUA iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika vijiji
vya Marumba na Morandi, wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma imeezua na kubomoa nyumba
62 za wananchi na kuwaacha wakiwa hawana mahali pa kuishi.
Taarifa za tukio hilo zinafafanua kwamba mvua hiyo ilianza
kunyesha majira ya saa 10 za jioni February 6 mwaka huu, ambazo ziliambatana na
radi huku upepo mkali ukianza kuezua mapaa ya nyumba hizo.
Walisema kufuatia hali hiyo, watu waliokumbwa na adha hiyo
walianza kukimbia huku na huko wakiwa wanapita kuomba msaada wa kujihifadhi kwa
majirani na ndugu zao.
Monday, February 8, 2016
AHADI YA MAGUFULI SHILINGI BILIONI 12.3 UENDESHAJI MAHAKAMA YATIMIA LEO
Sunday, February 7, 2016
ATIWA MBARONI KWA KUFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WATATU
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, limemtia mbaroni Kassim
Millinga (52) ambaye ni mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa
tuhuma za kuwabaka wanafunzi watatu wanaosoma darasa la sita shule ya msingi ya
Kibulang`oma iliyopo mjini hapa.
Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi
Mwombeji alisema kuwa tukio hilo limetokea kwa nyakati tofauti katika eneo la
Lizaboni jirani na shule hiyo wanayosoma wanafunzi hao, ambao wote wana umri wa
miaka 12 kila mmoja na majina yao yamehifadhiwa.
![]() |
| Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji. |
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa Millinga ambaye pia
anafanya kazi ya ulinzi kwenye kampuni ya ulinzi ya Ilonjezi iliyopo mjini
Songea, anatuhumiwa kwamba kwa nyakati tofauti tangu mwaka jana amekuwa
akiwarubuni wanafunzi hao kwa kuwapa pesa, chakula na nguo kisha kuwalazimisha
kufanya nao mapenzi kwenye nyumba anayoishi huku akiwatishia kutosema kwa mtu
yeyote kuhusiana na kitendo hicho anachowafanyia.
VURUGU ZAKWAMISHA UCHAGUZI CHUO KIKUU SONGEA
Na Mwandishi wetu,
Songea.
UCHAGUZI Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani Ruvuma, umeshindwa kufanyika kwa kile kinachodaiwa kuwa uongozi husika wa chuo hicho umekuwa ukiingilia na kutaka kupanga safu ya uongozi wanaoutaka wao, huku wanachuo wakishindwa kuwa huru kuchagua kiongozi wanayemtaka.
UCHAGUZI Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani Ruvuma, umeshindwa kufanyika kwa kile kinachodaiwa kuwa uongozi husika wa chuo hicho umekuwa ukiingilia na kutaka kupanga safu ya uongozi wanaoutaka wao, huku wanachuo wakishindwa kuwa huru kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo, kumesababisha vurugu za hapa
na pale katika eneo hilo la chuo, ambazo zilipelekea mmoja wa viongozi wa chuo
hicho ambaye ni mtawa aliyefahamika kwa jina moja la Magdalena, raia wa kutoka
nchi ya India kunusurika kipigo kutoka kwa wanafunzi wakati alipokuwa akitangaza
uchaguzi huo hautafanyika.
Habari zaidi kutoka kwenye chuo hicho zinaeleza kuwa, mapema
miezi mitatu iliyopita wanafunzi wa chuo hicho walitangaziwa kuwa mwanachuo
yeyote anayetaka uongozi achukue fomu ya kugombea, na hili lilitokana baada ya
uongozi uliokuwa madarakani kuisha muda wake wa utawala.
Wanachuo hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe,
waliwaambia waandishi wa habari kuwa baadaye mchakato wa kuwapata viongozi
uliendelea ambapo wagombea walijitokeza na kuanza kufanya kampeni za kuomba
wachaguliwe kwa nafasi walizoomba.
Friday, February 5, 2016
WALIOBOMOLEWA NYUMBA TUNDURU KUPISHA UJENZI WA BARABARA KULIPWA FIDIA ZAO
Na Steven Augustino,
Tunduru.
IMEELEZWA kuwa wahanga 280 ambao walibomolewa nyumba zao, kwa
lengo la kupisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika vijiji vilivyopo
kwenye tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hivi sasa wameweza
kutimiza vigezo vya kuishawishi serikali kulipwa fidia zao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoufikia mtandao huu, imefafanuliwa
kuwa wahanga hao ni kati ya wananchi 352 ambao walipeleka malalamiko yao, ya
kuomba kuongezewa fidia kwa madai kwamba awali hawakuridhishwa na malipo ya
fidia waliyolipwa awamu ya kwanza.
Taarifa hiyo ilitolewa na mwakilishi wa dawati la kusikiliza migogoro
kutoka makao makuu ya Wakala wa barabara hapa nchini (TANROADS), Gibson Mwaya
wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa wahanga hao, waliokuwa wamekusanyika katika
viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kwa ajili ya kufuatilia hatima
ya madai yao.
JE INAWEZEKANA HATI KUWA NA MAJINA YA WANANDOA WOTE ?
Na Bashir Yakub,
HAKIMILIKI katika
masuala ya ardhi, huhusisha umiliki wa ardhi
zenye hati. Umiliki huu hutoa wajibu na haki
fulani kwa mmiliki katika ardhi husika, na sio rahisi kudai
kwamba una hakimiliki katika ardhi kama hauna
hati.
Aidha tumezoea
kuona hati zilizo na jina la mtu mmoja
mmoja. Hii ni hata kwa wanandoa ambao
hudai mali husika zinatokana na jasho lao wote.
Lakini je unajua kuwa inawezekana hati
miliki ikawa na majina ya wanandoa wote
badala ya kuwa na jina la mmoja tu hasa baba ambao
ndio wengi hupenda majina yao yaonekane hapo
?. Jambo hili linawezekana na linaruhusiwa.
1. HAKIMILIKI YA
PAMOJA KUONDOA MGOGORO.
Kutoelewana ambako
mara kadhaa hutokea baada ya kifo cha
mmoja wa wanandoa, kunaweza kuondolewa
na umiliki wa ardhi wa pamoja. Ikiwa una
wasiwasi juu ya mustakabali wa mali
hasa ardhi huko mbele, ni vyema basi
ukachukua hatua ya kusajili kwa umiliki wa
pamoja.
Kama kiwanja / nyumba
ina hati yenye majina mawili, la baba na mama halafu
mmoja wao akafariki itakuwa ni vigumu ndugu
au mwingine yeyote mwenye nia mbaya kudai
umiliki wa kiwanja / nyumba hiyo.
Lakini hali itakuwa
tofauti iwapo hati ina jina la mmoja
na huyo huyo mmoja ndiye aliyefariki. Hivyo pale
pote ambapo ndugu walidhulumu mali za marehemu
hasa ardhi, ni pale ambapo kuna jina la
mmoja.
Mara nyingi fitina
huingia pale penye mwanya wa kufanya hivyo. Sio
rahisi fitina kuingia pasipo na mwanya. Kuweka majina
ya wanandoa wote kwenye hati za ardhi
ni hatua ya kuziba mwanya wa fitina.
Itawezekanaje ndugu au
mwingine mwenye nia ovu kudai umiliki wa ardhi
ya marehemu huku akijua kuwa, hati husika inalo
jina la mke pia. Sio rahisi hata kidogo.
Lakini pia umiliki
wa pamoja huondoa mgogoro pale panapokuwa
na talaka. Swali la kujiuliza je, mwanandoa fulani
amechangia chochote katika kupatikana kwa mali
huwa halipo ikiwa majina yote mawili
ya wanandoa yameonekana kwenye hati.
Subscribe to:
Posts (Atom)








