Na Kassian Nyandindi,
Mbamba bay.
BAADHI ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamekiasi chama hicho na kuhamia Chama
Cha Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichoeleza kuwa, wamechoshwa na sera za
Chadema ambazo zimekuwa zikichochea machafuko mara kwa mara hapa nchini.
Wafuasi hao ambao walikuwa 67 walieleza kuwa, hawana sababu
ya kuendelea kuwa katika chama hicho cha upinzani badala yake waliona ni heri
warejee kwenye chama mama, CCM ambako walikuwa tokea awali.
Hali hiyo ilitokea leo katika viwanja vya mji mdogo wa Mbamba
bay wilayani humo, kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Kamanda wa
Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa,
Cassian Njowoka.
Aidha katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa
wa wananchi wa mji huo, kelele na shangwe za hapa na pale zilirindima katika
viwanja hivyo huku wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi, wakiwapokea wenzao wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwa furaha wakati wanarudisha kadi zao za
chama hicho cha upinzani.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika kusikiliza mkutano
huo, ambao ulilenga kumsimika rasmi kamanda wa UVCCM wa kata ya Mbamba bay,
Kamanda wa Jumuiya hiyo wilaya ya Nyasa Njowoka alisema kuwa, jambo muhimu kwa
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni kujenga ushirikiano imara katika kufanya
shughuli mbalimbali za kimaendeleo, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
“Ndugu zangu nawasisitiza, tunapaswa wote kwa pamoja kujenga
wilaya yetu kwa faida ya baadaye, hatupaswi kubaguana au kujenga matabaka
yasiyokuwa na lazima katika jamii”, alisema.
Pia Njowoka alitoa ahadi ya vitanda 20, magodoro 20 na
mashuka yake ya kujifunika wagonjwa katika Hospitali ya wilaya ya Nyasa, ambayo
inakabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.
Vilevile katika Hospitali hiyo, alisema atawapatia kitanda
kimoja cha kujifungulia akina mama wajawazito ili kiweze kuwasaidia akina mama
hao, wakati wa kujifungua.
No comments:
Post a Comment