Wednesday, April 8, 2015

LITUNGURU AMCOS WASIOLIPA MIKOPO KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

LITUNGURU Amcos, ambacho ni chama cha wakulima wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimewataka wanachama wake kurejesha deni wanalodaiwa na benki ya CRDB shilingi milioni 36 ambazo walikopeshwa kwa ajili ya kununua pembejeo, ili waweze kuboresha mashamba yao ya tumbaku.

Mwenyekiti wa chama hicho Zainabu Baisi alisema kuwa mkopo huo, ulitolewa na benki hiyo katika msimu wa mwaka 2011/2012, hivyo mwanachama ambaye hajajiandaa kurejesha hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Alisema tayari orodha ya wadeni imeanza kuwasilishwa katika ofisi za watendaji wa vijiji na kata, kwa hatua zaidi na kwamba maafikiano hayo yamefikiwa baada ya bodi husika kuketi na kujadili hilo na baadaye kubaini kwamba, chama hicho kinakosa sifa ya kukopesheka kutokana na kutorejesha mikopo kwa wakati.


Baisi alisema hayo, alipokuwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika kijiji cha Mchoteka wilayani humo huku akisisitiza wanachama wake endapo hawatazingatia taratibu za kurejesha mikopo kwa wakati, wanahatarisha hata ustawi wa LITUNGURU Amcos kushindwa kuendelea kuhudumia wanachama wake kutokana na watu kutorejesha mikopo yao kwa muda muafaka.

No comments: