Baadhi ya Wadau wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakifuatilia mada kwa umakini katika semina ya wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika leo ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa
kuongeza uzalishaji katika zao hilo, ili waweze kujiongezea kipato na hatimaye
waweze kuondokana na umasikini.
Aidha wameaswa kuzingatia kununi bora za kilimo kwa kushirikiana
na wataalamu wa zao hilo, ili wafikie lengo la uzalishaji wa kahawa bora na
yenye kupata soko na bei nzuri mnadani.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alitoa rai hiyo leo
katika semina ya siku moja ya Wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika
kwenye ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa ambayo ilikuwa ikiendeshwa na benki
ya NMB tawi la Mbinga.
Ngaga alisema kuwa wakulima wa zao hilo, wanakila sababu ya
kuelimishwa juu ya kilimo bora cha kahawa ili waweze kuzalisha zaidi, na
kuifanya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla liweze kusonga mbele kimaendeleo.
“Tuelimishe wakulima wetu, waache kilimo cha mazoea tukiwa na
dhana hii ya kilimo cha biashara katika zao hili, ndugu zangu nina hakika tutafika
katika malengo yetu na kusonga mbele zaidi”, alisema Ngaga.
Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, zaidi ya
asilimia 90 ya mapato ya wilaya ya Mbinga hutokana na kilimo cha zao hilo,
hivyo wadau wa kahawa amewasisitiza kuendelea kuliboresha kwa manufaa ya kizazi
cha sasa na kijacho.
Awali akizungumza katika semina hiyo Meneja wa Kanda ya
kusini benki ya NMB, Lillian Mwinula alisema kuwa lengo kuu la benki hiyo ni
kuona kilimo cha zao hilo kinamwinua mkulima, ili aweze kuondokana na
changamoto mbalimbali ambazo hukabiliana nazo katika maisha yake ya kila siku.
Mwinula alisema benki hiyo inafanya kazi zake kwa uwazi na
kauli mbiu yake; Kilimo ni biashara, ikiwa ni lengo la kuhamasisha wakulima
waweze kuzalisha mazao kwa wingi na ubora zaidi.
No comments:
Post a Comment