Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
SERIKALI hapa nchini, imetakiwa kutoa kibali kwa taasisi
binafsi ziweze kushiriki kikamilifu kuchapisha nakala za rasimu ya pili ya katiba
inayopendekezwa, ili zisambazwe kwa wingi na kumfikia kila mwananchi kwa
wakati, hatimaye waweze kuisoma na kuielewa na baadaye waipigie kura ya maoni wakiwa
na taarifa sahihi.
Hayo yalisemwa na mtafiti wa maswala ya katiba hapa nchini,
Gelin Fuko kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu wakati alipokuwa kwenye
mkutano wa hadhara Mbinga mjini mkoani Ruvuma, uliofanyika kwenye viwanja vya
soko kuu mjini humo.
Aidha Fuko aliwataka wananchi wakati utakapofika katika
maeneo yao, wajiandikishe kwenye daftari la wapiga kura jambo ambalo
litawafanya waweze kuingia kwenye mchakato huo, wa kuipigia kura rasimu hiyo.
“Ndugu zangu msidanganyike kuwa umekumbukwa ilhali hata
hujasoma katiba hii inayopendekezwa, nawaombeni kabla ya kuipigia kura hakikisheni
umeiosoma na kuielewa ili muweze kutoa maamuzi yaliyo sahihi”, alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi nao kwa nyakati tofauti
walitoa maoni yao katika mkutano huo, ambapo walionesha kuiponda rasimu hiyo ya
pili ya katiba wakisema kuwa baadhi ya Wabunge wa bunge la Jamhuri ya muungano
wa Tanzania, wameichakachua katiba hiyo na kuingiza maoni yao na sio
yaliyopendekezwa na wananchi.
Walisema hali hiyo imetokana na serikali iliyopo madarakani,
kunga’ng’ania mfumo ambao wananchi hawaridhishwi nao hivyo katiba hiyo inanyima
haki wananchi kikatiba, na kutaka kupitisha mambo kiujanja ujanja.
Kadhalika walifafanua kuwa wao wanachotambua ni kwamba maoni ya
awali yaliyotolewa kupitia timu ya Jaji Warioba, ndiyo wanayoyatambua lakini
wanaishangaa serikali kuingiza maoni ya kwake ambayo yanalenga kuwavuruga
wananchi.
Hata hivyo kituo cha sheria na haki za binadamu, kinaendelea
na ziara yake ya kikazi kutoa elimu kwa wananchi juu ya rasimu hiyo ya katiba hapa mkoani Ruvuma, katika wilaya ya Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru.
No comments:
Post a Comment