Na Mwandishi wetu,
Songea.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Waandishi wa habari mkoani
Ruvuma jana wamejikuta wakifanya kazi katika mazingira mgumu, baada ya mmoja wa
Ofisa kutoka idara ya usalama wa taifa hapa nchini, kuwazuia waandishi hao
wasitekeleze majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Ofisa usalama huyo aliwazuia wasiweze kupiga picha, na
kuandika taarifa za uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa, zilizofanyika jana kwenye
uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Aidha aliwashangaza waandishi hao pale alipofikia hatua ya
kutamka kwamba wasitekeleze majukumu yao ya kazi, mpaka mgeni rasmi Dokta Alli
Mohamed Shein atakapokwenda kuketi jukwaani jambo ambalo wanahabari hao walimpuuza
na kutumia mbinu mbadala katika kuandika habari, na kupiga picha za tukio hilo.
Kadhalika Ofisa usalama huyo alionekana kutaka kuvunja maadili
yake ya kazi hasa pale, alipofikia hatua ya kuwafokea waaandishi hao na
kuwaambia kwamba atawadhalilisha kwa kuwaweka mahabusu kama hawataondoka katika
eneo la tukio hilo la Mwenge.
Vilevile aliendelea kuonesha dharau akiwaambia kwamba haoni
wanachokifanya, hivyo waondoke haraka kabla hajachukua hatua ya kuwaita askari
polisi ili watiwe nguvuni kama alivyokusudia kitendo ambacho waandishi
waliendelea kumpuuza na kufanya kazi zao kama kawaida.
Mwandishi wa habari Crecensia Kapinga ambaye anaandikia
gazeti la Majira, licha ya kuingilia kati na kumweleza ofisa usalama huyo
kwamba hao anaowafukuza ni waandishi wa habari, bado alionekana
kutomwelewa huku akimjibu kwamba yeye
hatambui kazi zao na waondoke mara moja kabla hajawaitia polisi.
Pamoja na mambo mengine waandishi wa habari mkoani hapa,
wamelaani kitendo hicho kilichofanywa na ofisa huyo wa serikali, na kutaka
vitendo vya kuzuia waandishi kufanya kazi zao kwa uhuru viachwe mara moja kwani
tasnia ya habari nayo inamchango mkubwa katika taifa hili.
No comments:
Post a Comment