Watoto wakisoma chini ya mti. |
Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
KAMANDA wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, Cassian Njowoka amesikitishwa na
kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu wilayani humo kushindwa kutatua tatizo la
ujenzi wa shule ya msingi Linda, ambayo imeezuliwa na upepo kitendo ambacho
kinasababisha wanafunzi kukosa masomo darasani.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hivi sasa wanalazimika
kusomea chini ya miti ya mikorosho, hali ambayo imekuwa ikiwapa kero kubwa
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nyakati hizi za masika.
Masikitiko hayo aliyatoa wakati alipokuwa kwenye ziara yake
ya kuwasimika makamanda wa kata wilayani humo, ambapo alipofika katika kata ya
Kilosa alielezwa tatizo la shule hiyo kuezuliwa na upepo Julai 11 mwaka jana.
Njowoka alisema ni jambo la kushangaza kuona shule hiyo
imekaa kwa muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati, jambo ambalo alifafanua kuwa ni
uzembe uliokithiri ambao haupaswi kuvumiliwa hivyo aliwaasa viongozi wa wilaya
ya Nyasa, kujenga tabia ya kutembelea shule za msingi na sekondari ili kubaini
changamoto mbalimbali na kuzipatia utatuzi kwa wakati.
Alisema yeye akiwa Kamanda wa vijana, tatizo hilo limemgusa
kwani UVCCM kamwe haiwezi kuona chipukizi wake ambao baadaye watakuwa wanachama
wake wanapata shida, hivyo aliamua kuchangia bati 90 ili zisaidie kuezekea
shule hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Linda wilayani Nyasa, Essau Ndunguru alieleza kuwa jengo hilo lililoezuliwa
ni la vyumba vitatu, ambalo lilikuwa likitumika kusomea watoto wa darasa la
nne, tano na la saba ambapo takribani wanafunzi 140 wanakosa sehemu ya kusomea
kutokana na kukumbwa na maafa hayo.
Ndunguru alifafanua kuwa, kutokana na kukosa fedha kwa muda
mrefu za kuendelea na ujenzi huo ndio kumesababisha kukwama, na hivyo watoto hao
kuendelea kukumbwa na adha hiyo.
“Watoto hivi sasa wanasomea chini ya miti ya mikorosho, ambayo
ipo hapa jirani na shule yetu kutokana na jengo hili walilokuwa wakilitumia
kusomea kuezuliwa na upepo mkali, tunaiomba serikali na wadau mbalimbali waone namna
ya kutusaidia juu ya kumaliza tatizo hili ili tuweze kuondokana na usumbufu
tunaoupata sasa”, alisema Ndunguru.
Hata hivyo mwalimu huyo aliwaasa wazazi na walezi wa kijiji
cha Linda kujitokeza bila kusukumwa kuchangia nguvu zao, pale wanapotakiwa ili
kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu jambo litakalowafanya
waweze kuishi jirani na mazingira ya shule tofauti na ilivyo sasa, hulazimika
kuishi uraiani.
No comments:
Post a Comment