Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste
Mapunda,
PASAKA ni sikukuu ya
kusherehekea “ushindi wa Yesu” dhidi ya mauti, dhidi ya maovu ya kila aina
yanayomshambulia mwanadamu kwa wale wanaomwamini. Yesu amefufuka kweli, kweli kama
alivyosema, hayupo kaburini yu hai.
Ujumbe huu ni mzito na
wa kushitua ulimwengu wote, hasa kwa waliowakristo na wasiowakristo.
Jumapili ya Pasaka nilisherehekea
Parokiani Manzese na ibada ilikuwa na mahudhurio makubwa, pamoja na hamasa ya
hali ya juu. Ibada siku zote zinatujenga sana kama mashahidi wa ufufuko wa
Kristo.
Jumatatu ya Pasaka nilikuwa
na ratiba ya kuhudhuria misa ya saa tatu, ambayo ilikuwa ni ya ubatizo na ndoa.
Lakini nikajikuta nasukumwa kwenda kuhudhuria misa ya saa moja, ambayo ilikuwa
ni ya wanaumini wa kawaida. Nilipofika Kanisani nilimkuta Padre na mwanashirika
mwenzangu, Padre Alex Mutasingwa ambaye
alikuwa kiongozi ibada.
Kilipofika kipindi cha mahubiri,
Padre Alex alinichoma sana pale alipozungumzia juu ya matumizi ya rushwa ya
fedha waliyohongwa maaskari, waliokuwa wakilinda kaburi la Yesu, ili wadanganye
kwamba “walipokuwa wamelala basi wafuasi wake walikuja kumwiba.”
Ufufuko wa Yesu ulikuwa
ni tishio na mwiba kwa uongozi wa Kiyahudi, kwani wao hawakusadiki kama kweli
Yesu alikuwa ni mwana wa Mungu, ambaye angefufuka siku ya tatu.
Wakuu wa Mayahudi baada ya
kupata habari kwamba Yesu hayumo kaburini, walifadhaika sana na hivyo kutafuta
haraka sana, njia ya kupotosha ukweli wa ufufuko huo ambao ulikuwa n ushindi dhidi
ya fitina yao ya kumuua.
Mbinu chafu waliyopanga
ni pale viongozi hao wa Mayahudi, kuwaambia
maaskari polisi kwamba “ninyi chukueni pesa hii na mseme kwamba tulipokuwa tumelala wafuasi wake walikuja kumwiba
usiku.” Na viongozi hao waliapa kuwalinda maaskari hao ili wasisumbuliwe na
jamii.
Hadi leo hii dunia na
jamii yetu, askari polisi wanaendelea kutumiwa ili kupotosha ukweli kwa rushwa ya pesa. Je, hii inatokana
na laana ya pesa iliyomtoa Yesu mwenyewe?
“UKWELI DAIMA UTASHINDA” kwani
Yesu hatimaye alijitokeza kwa wafuasi wake na salamu ya amani kwenu msiogope, akajidhihirisha
kwamba hajaibiwa bali amefufuka katika wafu. Yesu anatibu sumu ya rushwa kwa
kutumia ukweli kwamba yeye amefufuka. Habari hii ni mbaya kwa maadui.
Maandiko matakatifu
huwalaani na kuwakaripia Mahakimu na Polisi ambao wanadhamana kubwa ya kusimamia,
HAKI NA
UKWELI BILA KUPENDELEA. Hii inatokana na ukweli kwamba Mungu wa Wana
wa Waisraeli, hapendelei nyuso za watu (kumb 10:17). Mwalimu Nyerere alisema Rushwa ni adui wa haki.
Inaonekana wazi kwamba
rushwa ya maaskari, ilianza sikukuu ya ufufuko wa Bwana. Na hii yote walifanya ili
kupotosha ukweli kwamba, Yesu amefufuka tukio ambalo lilikuwa ni aibu kwa
viongozi wa Kiyahudi, lakini kwa waliomwamini ulikuwa ni ushindi wa
kishindo.
Mungu bado
anaendelea kuichukia rushwa,
anapowakaripia viongozi na wenye madaraka kwamba “wewe usipokee rushwa, huwapofusha hao waonao na kuyapotosha maneno ya wenye haki” (Kumb
23:18). Pasaka hutufundisha kwamba rushwa inauwezo wa kupotosha ukweli hata
hivyo ilishindikana kabisa.
Je, katika nchi yetu
propganda za kisiasa ni sehemu ya kuupotosha ukweli? Kiongozi anayepokea rushwa
hukosa heshima, na baraka ya kuwatumikia watu waliompa dhamana.
Viongozi wa ngazi zote
katika jamii yetu yaani serikali, vyama vya siasa, taasisi na madhehebu ya dini
ni jukumu letu kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa haki, hasa haki kwa maskini.
Nabii Isaya anaonya kwa kusema bayana
kwamba “viongozi wa Israeli hawajali chochote kwa dhiki za
wanyonge, huwanyang’anya haki zao.” Je hapa nchini hali ipoje?
Wajibu wa Manabii
kuwaonya viongozi wa jamii, juu ya haki ya wanyonge inayoathiriwa na rushwa.
Nikirudi katika tafakari
ya Padre Alex Mutasingwa, Jumatatu ya Pasaka kanisani Manzese ilinichoma sana
wakati aliposisitiza juu ya ujasiri wa viongozi kusimamia ukweli. Siku hizi
katika jamii yetu baadhi ya viongozi wapo tayari kupokea rushwa na kutoa viapo kwa Mungu na jamii kwa
ujumla, ili kuuangamiza ukweli na haki kama walivyofanya siku ya ufufuko wa Yesu Kristo.
Ni mara ngapi watu
wanasimama kusema uwongo hata Mahakamani, ili kupotosha na kupindisha ukweli?
Leo ukiichunguza nchi yetu unakuta mivurugano ya kila aina, na wananchi wamejaa
malalamiko na huzuni za kila aina.
Maovu na machafuko
yametawala kila kukicha. Matumizi ya rushwa yanaonekana kuliangamiza taifa letu,
bila watawala kujua cha kufanya. Swali langu ni hili kwa nini
viongozi wahusika wanaogopa
kuusimamia ukweli?
Mtume Petro mara baada
ya kwenda kaburini na kubaini kwamba Yesu kweli alikuwa amefufuka, aliamini. Kuamini
huku kulimpatia nguvu ya kwenda kwa wale
maadui wa Yesu waliomuua na kueneza uwongo kwamba alikuwa ameiibiwa.
Petro anapata ujasiri wa
kuwaambia ukweli kwamba, “yule aliyefufuka
msipoteze muda wa kutafuta tafuta ni nani, kwani ni yule yule,
mliyemdharau, mliyemkejeli, mliyemtukana na kumdhihaki na mliyemwambia
msalabani, ni Yesu kristo aliyefufuliwa
na nguvu ya Mungu.
Katika hili Petro naye
alikuwa amejipatia ujasiri wa kuufika ukweli, kwa sababu “ukweli unakuweka
huru” (Rumi 8:31).
Tunapoendelea kushereka
sikukuu hii ya Pasaka, ambayo ni sikukuu ya ushindi wa Yesu dhidi ya uwongo na
maovu basi nasi tubadilishwe na nguvu ya
ufufuko wa Yesu Kristo.
Nchi yetu inayopita
katika kipindi hiki kigumu hasa katika nyanja ya kiuchumi, kijamii, kiutumaduni,
kiimani na kisiasa juu ya suala la katiba mpya na mitifuano iliyopo ya mahakama
ya kazi, tunahitaji iongozwe na ukweli.
Namaliza kwa kusema
“nchi yetu itakombolewa na viongozi wenye ujasiri wa kusimamia ukweli toka
mwanzo hadi mwisho, bila kuyumbishwa na pesa wala vyeo kama walivyoonyesha Maaskofu
wa Jukwaa la Wakristo, katika suala la upigaji kura ya hapana kwa katiba
pendekezwa.
Halikadhalika Yesu na
Petro wanatufundisha kwamba rushwa ni kansa ya roho na akili, ni lazima tutumie
nguvu ya Mungu katika kuitibu.
Nawatakieni Pasaka njema
yenye amani, furaha, upendo, matumaini na maisha mapya.
Mwandishi wa makala haya
anapatikana kwa barua pepe; Frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment