Thursday, April 30, 2015

MWAMBUNGU ATAKA WANANCHI WA KITONGOJI CHA MANGAWAGA NYASA WASIHAMISHWE

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ametoa agizo la kuutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani humo, kusitisha mara moja mchakato wa kuwahamisha wakazi wa kitongoji cha Mangawaga kijiji cha Mkalole kata ya Kilosa wilayani humo, mpaka serikali itakapotoa maelekezo mengine.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa mkoa, liliwasilishwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.

“Ndugu zangu nimeagizwa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ni marufuku kuhama endeleeni kuishi hapa kijijini mpaka serikali itakapotoa maelekezo mengine, hivyo ondoeni wasiwasi katika jambo hili ninalowaambia”, alisema Njowoka.


Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa kijiji cha Mkalole Romward Msuha alisema kuwa kijiji na vitongoji vyake kilianzishwa mwaka 2000 na kutambuliwa kisheria, hivyo wanaushangaa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa kutaka kuwahamisha bila kufuata taratibu husika ikiwemo ulipwaji wa fidia.

Msuha alisema idara ya maliasili na mazingira wilayani humo, ndiyo inayotumia nguvu ya kutaka kuwahamisha kwa kile alichoeleza kwamba, wananchi hao wanaishi katika eneo la hifadhi hivyo inabidi waondolewe.

Alisema mnamo mwezi Januari mwaka huu, viongozi wa idara hiyo walikwenda kijijini hapo na kubandika mabango ya kuhimiza kuhama wananchi hao, ifikapo mapema mwezi wa tano mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema baada ya kuona hilo, kijiji kilituma wajumbe wanne kwenda kupeleka malalamiko yao kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mwambungu juu ya tatizo hilo na baadaye aliwaahidi atatuma tume ya kuja kulichunguza, ili liweze kutekelezwa kwa haki bila wananchi kunyanyaswa.

Naye Katibu wa tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mkalole, Thadei Mahungu alieleza kuwa wananchi wanataka jambo hilo lipatiwe ufumbuzi wa amani na sio kujenga mgogoro, wenye kuhatarisha amani baadaye.

“Jambo hili tunahitaji tufikie muafaka mzuri kwa njia ya amani na hatutaki kuondolewa kwa nguvu bila kufuata taratibu za kisheria, kwani wengi wetu tumeweka makazi yetu na mashamba kwa muda mrefu ambayo tumezalisha mazao ya aina mbalimbali, ya chakula na biashara”, alisema Mahungu.


Katibu huyo alifafanua kuwa wananchi wanaoishi katika eneo hilo, walianza kuishi kabla ya mfumo wa vijiji kuanzishwa hapa nchini, na kwamba waliongeza kuwa ni kosa na hawaoni sababu ya wao kuhamishwa, bila kuandaliwa sehemu nyingine ya kwenda kuishi.

No comments: