SISI maaskofu na wachungaji kutoka makanisa mbalimbali
tumeshtushwa na kusikitishwa kwa taarifa ya ugonjwa wa Askofu na mtumishi
mwenzetu Josephat Gwajima ambaye tarehe 27/03/2015 alifika kituo cha polisi cha
kati kuitikia wito wa polisi uliomtaka kwenda kujibu shutuma za kutumia lugha
ya matusi kwa kardinali Pengo.
Tumepata fursa ya kutafakari na kujadili kwa kina hali iliyompata
Askofu mwenzetu hasa baada ya kuzingatia kuea Askofu Gwajima alifika polisi
akiwa mzima na mwenye afya njema lakini wakati wa akihojiwa na polisi, hali
yake ilibadilika ghafla kiasi cha kupelekea yeye kulazwa hospitali ya TMJ
akiugua tena kwenye wodi ya wagonjwa mahututi yaani (ICU) katika chumba cha
uangalizi maalum.
Maswali yetu makuu ni kitu gani kimempata mwenzetu? Tunajiuliza,
je vyombo vya usalama vimekua sio sehemu salama kama zamani?
Tukiwa bado tunatafakari hill, tumeshtushwa tena baada ya kupata
taarifa ya kuwa Wachungaji Wasaidizi wa Askofu Gwajima pamoja na walinzi wake
waliokuwepo hospitalini hapo kwa ajili ya kumuuguza nao pia wamekamatwa kwa
tuhuma za. kutaka kumtorosha Askofu Gwajima.
Jambo hili linashangaza zaidi maana wachungaji wale wale waliokuwa
naye akiwa mzima wa afya wakati anaelekea polisi ndio wale wale wanatuhumiwa
kutaka kumtorosha akiwa mgonjwa.
Ni jambo la kushangaza na lisiloingia akilini kuwa wasaidizi hao
wa Gwajima walitaka kumtorosha wakati Gwajima kama angekua na nia hiyo
angekwisha fanya hivyo mana alikuwa na uwezo wa kutoroka alipokua Arusha kwenye
kikao cha Maaskofu wakuu wa makanisa ya Kipentekoste ambao alipata taarifa za kuitwa
Polisi.
Isitoshe Gwajima aliitija wito na kwenda polisi mwenyewe kwa miguu
yake bila kushurutishwa, wala hakufikishwa polisi kwa nguvu.
Swali: Kama alikua anaona ugumu wa kutoroka wakati hakuna polisi
anayemlinda na huku akiwa mwenye afya tele, itakuaje rahisi kutoroshwa leo
akiwa mahututi na akiwa kwenye ulinzi mkali wa polisi? Mbona hii
inastaajabisha?
Jambo jingine linalotupa shida ni kuhusu mlalamikaji wa kesi hii
inayomkabili Askofu Gwajima. Tumeelezwa na wasaidizi wa Askofu Gwajima kuwa
pale polisi walielezwa kuwa aliyefungua kesi hii sio Pengo ila mtu mmoja
aitwaye Aboubakar.
Kwa ufahamu wetu juu ya sheria unatutuma kuamini kuwa Aboubakar
sio MTU sahihi wa kufungua kesi hiyo sababu hawezi kutuonyesha ameumizwa kiasi
gani na matamshi ya Askofu Gwajima.
Isitoshe, Kardinali Pengo mwenyewe ametamka katika Ibada yake ya
Jumapili hii ya tarehe 29/03/2015 kuwa amemsamehe Gwajima, yupi tena mwenye
uchungu wa kumzidi Kardinali Pengo?
RAI YETU:
Rai yetu ni kwamba, ni vizuri serikali pamoja na vyombo vyake vya
usalama vikatumia weledi katika kushughulikia mambo ya kidini na viongozi wake
kwani yanaweza kusababisha chuki dhidi ya serikali na pia kupelekea mpasuko
mkubwa wa kidini katika jamii yetu iliyo na historia nzuri ya umoja na
mshikamano na ushirikiano katika matukio yote ya kimaisha.
Tunaomba serikali isaidie kuondoa mkanganyiko huu na busara kubwa
itumike ili kuepusha uvunjifu wa Amani katika jamii.
MAAMUZI YETU:
Hili linazungumzika, maana hata hivyo tumeshaazimia kukutana na
IGP ili kupata suluhisho juu ya jambo hili.
Kwa niaba ya maaskofu na wachungaji:
Mwenyekiti: Askofu Dr. Mgullu Kilimba
Katibu: Askofu Dr. Dramas Mukassa
Na mwandishi;
F.A.K
30/03/2015
No comments:
Post a Comment