Adolph Kumburu, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake na Wadau wa zao hilo, hapa nchini. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Adolph Kumburu,
amesema kuwa msimu wa mavuno ya zao hilo hapa nchini umefunguliwa mapema mwezi
Aprili mwaka huu, kutokana na baadhi ya maeneo ambayo yanawahi kuiva zao hilo
wakulima waweze kuuza kahawa yao mapema bila kuchelewa.
Aidha msimu huu wa mwaka 2015/2016 bodi imefanya makadirio ya
kukusanya tani 60,000 tofauti na msimu wa mwaka 2014/2015 ilikadiria kukusanya
tani 44,000 lakini haikufikia lengo hilo, badala yake ilikusanya tani 43,000 tu
jambo ambalo alifafanua kuwa lilitokana na baadhi ya maeneo hapa nchini zao
hilo kushambuliwa na wadudu waharibifu, na kusababisha kushindwa kufikia malengo
husika.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi huyo, alipokuwa kwenye mkutano
wa Wadau wa zao la kahawa mkoani Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa Jumba la
maendeleo wilayani Mbinga mkoani humo.
Kumburu alieleza kuwa umekuwa ni utaratibu wa bodi, kufanya
mkutano kama huo na wadau wa zao la kahawa ili kupata fursa ya kutathimini kama
kuna tatizo lolote lililojitokeza katika msimu uliopita, na kuweka mikakati
madhubuti ili isiweze kujirudia tena katika msimu ujao.
Vilevile katika mkutano huo, Mkurugenzi huyo aliziagiza
Halmashauri za wilaya hapa nchini, maeneo ambako kahawa inazalishwa kuhakikisha
kwamba inatunga sheria za uendeshaji wa mitambo ya kuchakata kahawa (CPU), ili
zao hilo liweze kuzalishwa katika ubora.
Alifafanua kuwa wakulima kwanza, wapate uhalali wa kutumia mitambo
hiyo kwa kile alichoeleza kuwa kahawa nyingi huingia katika soko ikiwa na ubora
unaokubalika, na kwa msimu uliopita mikoa ya ukanda wa Kusini na Magharibi wakulima
ndio walioongoza kuzalisha zao hilo katika viwango vyenye ubora.
“Wakulima jitahidini mchakate kahawa wenyewe, huku
mkizingatia kanuni za kilimo bora ikiwemo taratibu za uzalishaji wa zao hili la
kahawa, ili tuweze kukuza kipato chetu na Taifa letu kwa ujumla”, alisema
Kumburu.
Kadhalika Kumburu aliongeza kuwa takwimu za uzalishaji zao
hilo hapa nchini zinaonesha kushuka kila mwaka, kutokana na wakulima wengi wanaozalisha
kahawa wamekuwa hawatumii pembeo za kilimo ipasavyo.
Pamoja na mambo mengine, alisisitiza kuwa ushuru unaokatwa na
Halmashauri mnadani Moshi kwa kila kilo ya kahawa inayouzwa, asilimia 20
inapaswa kurudi shambani kwa mkulima kwa lengo la kuboresha zao shambani, ili
mavuno yaweze kuongezeka mara dufu zaidi.
Alisema hakuna sekta ya kilimo duniani, ambayo inaweza
kusonga mbele bila kuingiza mtaji wa kutosha shambani hivyo kuna kila sababu
katika eneo hili muhimu, kutazamwa kwa undani na kuweza kuongeza uzalishaji.
Hata hivyo aliwataka wataalamu wa kahawa waache kukaa
maofisini, waende kwa wakulima kutoa maelekezo na kusimamia kanuni bora za
kilimo cha zao hilo ili kumsaidia mkulima, aweze kusonga mbele na sio kunufaika
watu wachache.
No comments:
Post a Comment