Na Kassian
Nyandindi,
WAKULIMA wanaozalisha zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma wamesema wanamshangaa Mbunge wao wa Jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence
Kayombo kwamba hakuna mkulima anayelalamika juu ya wizi wa fedha baada ya
kahawa yao kuuzwa mnadani Moshi, hivyo wamemtaka afute kauli hiyo na
kushughulikia matatizo ya wananchi wa jimbo hilo, na sio kukaa kupinga
malalamiko yanayotolewa na wananchi wake huku akijua fika kufanya hivyo ni kuendelea
kuitesa jamii.
Kwa nyakati tofauti walisema wamekosa imani naye baada ya Mbunge
huyo hivi karibuni kusikika kwenye vyombo vya habari, TV na Magazeti akikanusha
na kusema wakulima hao wamenufaika na mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) na hakuna aliyeibiwa fedha, ambapo ni muda mrefu sasa umepita pamoja
na kufikishiwa malalamiko hayo mezani kwake juu ya wizi waliofanyiwa wakulima hao
lakini hakuna hatua aliyochukua huku wakiongeza kuwa, huenda anamaslahi yake
binafsi ndio maana amekuwa akitumia muda mwingi kutetea jambo hilo.
Walifafanua kuwa umefika wakati sasa, kiongozi aliyechaguliwa
na wananchi kuacha tabia ya kutetea watendaji wa serikali ambao ni wezi
wakiwaibia wakulima wanyonge na endapo ataendelea kufanya hivyo, ni sawa na
kuwatesa wapiga kura wake na kuwanyima fursa za kimaendeleo kwa faida ya kizazi
cha sasa na baadaye.
“Huyu Mbunge sisi tunamshangaa sana, anafikia hatua
anadanganya watu kupitia vyombo vya habari kwamba hakuna mkulima anayelalamika
katika jimbo lake ameibiwa fedha baada ya kahawa kuuzwa mnadani yeye anawezaje
kuthibitisha hili, hivyo asubiri mwarobaini wake ataupata uchaguzi mkuu ujao”,
walisema.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa,
Mbunge Kayombo amefikia hatua ya kutoa kauli hizo baada ya Mkurugenzi wake,
Hussein Ngaga na viongozi wa vyama vya ushirika, kulalamikiwa na wakulima wa kahawa wilayani Mbinga kupitia vyombo
vya habari kuwa wanadaiwa kuwaibia shilingi milioni 783,399,412 katika sehemu ya
kahawa zao ambazo waliuza huko mnadani Moshi.
Wakulima hao ni wale ambao walikopeshwa fedha shilingi
bilioni 2 na shirika hilo la NSSF kupitia vyama vyao vya ushirika (AMCOS) vilivyopo
wilyani humo, ambapo lengo la shirika lilikuwa ni kutoa mikopo yenye gharama
nafuu kwa wakulima wadogo wadogo ambao wamejiunga kisheria katika vikundi,
hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na waondokane na umasikini.
Malalamiko haya yanafuatia pia, Mkurugenzi huyo kuingilia kati
na kupangia matumizi ya fedha juu ya mkopo huo ambao wakulima walikopeshwa,
jambo ambalo mpaka sasa amekuwa hataki kutoa hata mwenendo wa fomu ya mauzo ya
kahawa zao (Account Sale) ili wakulima waweze kujua hatma ya kahawa yao jinsi gani
ilivyouzwa huko mnadani.
“Tumekuwa tukinyimwa hata mwenendo wa matumizi ya fedha zetu tulizokopeshwa
na NSSF ambazo ziliingizwa katika akaunti zetu za vyama vya ushirika (Bank
Statement) ili tuweze kujua zimetumikaje, kwa sababu wakati wa manunuzi ya
kahawa mkurugenzi huyu alikuwa akitupangia matumizi tunakwenda kuchukua fedha
benki mpaka ruhusa itoke kwake na kiasi anachotaka yeye, sasa tunahoji hivi
kweli hizi ndizo taratibu na sheria za vyama vya ushirika zinavyosema?”,
walihoji.
Pamoja na mambo mengine, wakulima wanaolalamikia juu ya hali
hiyo wanatoka katika vyama vinne vya ushirika ambavyo ni Mahilo, Ngaka, Ngima
na Pilikano ambapo hata viongozi wao wa ushirika nao wanalalamikiwa kwamba wameshirikiana
na Mkurugenzi Ngaga kwa namna moja au nyingine kuhujumu fedha hizo za wakulima
wa kahawa, huku wakiiomba serikali kuingilia kati ili haki zao ziweze kupatikana.
KAYOMBO ARUSHIWA KOMBORA
Wakulima hao ambao walionekana kuendelea kujawa na jazba,
waliibua jipya huku wakiendelea kumrushia kombora Mbunge wao Kayombo wakisema kuwa,
mnamo mwezi Agosti mwaka 2012 alianzisha umoja wa wakulima wa kahawa
unaofahamika kwa jina maarufu la; Mbinga Umoja Coffee Association, ambao
ulilenga wakulima wa kahawa wilayani humo waweze kufanya biashara ya kuuza
kahawa yao kwa bei nzuri nchi za nje.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, vikundi ambavyo
vilisajiliwa na idara ya maendeleo ya jamii wilayani hapa, vilichangishwa fedha
nyingi na kuingizwa ndani ya umoja huo lakini hakuna maendeleo yaliyozaa
matunda.
Mbunge huyo anashutumiwa kwamba, alikuwa akitumia hata fedha
za mfuko wa jimbo kuendeshea umoja huo huku akitambua anakiuka taratibu na ni
matumizi mabaya ya fedha za wananchi, ambazo ilibidi zikafanye shughuli husika.
Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Mwenyekiti wa umoja
huo, Aidan Turuka alithibitisha juu ya Kayombo kuwapatia fedha shilingi milioni
7,700,000 kutoka katika mfuko huo wa jimbo, ambazo hutolewa na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi.
Jitihada zilizofanywa na mwandishi wetu, zilifanikiwa kupata
bank statement yenye kuonyesha siku fedha hizo zilipoingizwa kwenye akaunti ya
umoja huo, namba 61710000760 benki ya NMB tawi la Mbinga.
Tarehe 22 mwezi Juni, mwaka 2012 fedha hizo ziliwekwa kwenye
akaunti hiyo kupitia mfumo wa hundi na baadaye kutolewa kidogo kidogo, kwa
ajili ya matumizi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya umoja.
Walifafanua kuwa baada ya umoja huo, kukusanya kahawa nyingi
za wakulima ambazo zilikobolewa kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga (MCCCO) na
kuhifadhiwa katika ghala la Makambako mkoani Njombe kwa muda mrefu, huku Mbunge
huyo akiwadanganya wakulima kuwa anatafuta masoko nje ya nchi ili ikauzwe kwa
bei nzuri na kuwazuia wasipeleke mnadani Moshi.
Lakini mwishoni alikosa soko na kusababisha hasara kwa
wakulima, na kulazimika kahawa kuuzwa huko mnadani kwa bei ya chini kutokana na
kukaa muda mrefu bila kuuzwa huku mnada wa mauzo ukiwa umepita, jambo ambalo
lilisababisha wakulima wengi wilayani Mbinga, kupata hasara na kudaiwa na benki
ya NMB ambako walikopa fedha kwa ajili ya kuendeshea biashara hiyo ya kahawa.
Baadhi ya wakulima wamepata hasara kufuatia mali zao ambazo
waliwekea dhamana benki, kupigwa mnada na kuuza kwa bei ya hasara ili kufidia
deni walilokuwa wakidaiwa na benki hiyo.
Pia kufuatia hali hiyo imefanya umoja huo ufe kifo cha mende
na Kayombo kubuni mbinu mpya kukimbilia Shirika la NSSF kushawishi, ili wakulima
wakopeshwe fedha kwa ajili ya kununulia kahawa na leo wanaibiwa tena ndio maana
kumekuwa na mwendelezo wa malalamiko ya hapa na pale.
Kutokana na mambo hayo wakulima wengi wa kahawa wilayani
humo, wamesema wamechoshwa na kauli za Mbunge huyo kutetea masuala ambayo
hayana tija kwao, hivyo wameapa kamwe hawataweza kuendelea kuvumilia mateso
wanayopata sasa na yeye akiendelea kutetea watu wanaowaibia wakulima wanyonge,
ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi jembe la mkono kuzalisha mazao shambani
ili maisha yao yaweze kusonga mbele.
Hivi karibuni alipotafutwa Kayombo ili aweze kuzungumzia juu
ya madai haya alisema kuwa, anashangaa kwa nini malalamiko hayo yanatokea
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu hivyo haoni haja ya wao kumuadhibu.
No comments:
Post a Comment